November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Mwasa: Tumieni matokeo ya Sensa suala la malezi Mbadala

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Morogoro

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwasa amelishauri Jukwaa la Kitaifa la Malezi Mbadala kutumia matokeo ya Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2022 kuwa dira ya kupanga mikakati katika suala la malezi kwa rika la watoto wa chini ya miaka 8 wanaoishi mitaani linaloongezeka.

Mwasa ametoa wito huo jana Disemba 10, 2022 wakati akifunga Kikao kazi kati ya Serikali na wadau mkoani Morogoro.

Ameshauri wadau na washiriki wa Jukwaa la Kitaifa la Malezi wanapaswa kutumia taarifa za matokeo ya Sensa ili kugundua ni kundi rika gani linaloongezeka kwa kasi na kuhitaji Malezi Mbadala.

“Niwashauri mjikite kwenye kuangalia matokeo ya Sensa ya mwaka huu, muangalie kundi rika gani limekua kubwa au linakua kwa kasi sana mfano kundi rika la miaka 8 kushuka chini limeongezeka sana, Mfano kwa robo muhula matukio ya ubakaji hapa mkoani Morogoro yalikua 52 kwahiyo ukatili dhidi ya watoto kati ya umri wa miaka Miaka 8 kushuka chini ni mkubwa sana kwahiyo tunapoangalia namna ya kusaidia malezi ya watoto, Tuangalie namna ya kuzuia visababishi,” amesema Mwasa.

Mkuu wa Mkoa Mwasa, amesema Umaskini ni miongoni mwa sababu kubwa inayosababisha watoto kuhitaji malezi mbadala, kwani wapo watu hutelekeza watoto kwa sababu wamekosa uwezo wa kuwahudumia.

“Sababu zinazoleteleza watoto kuhitaji malezi mbadala ni nyingi, lakini miongoni mwazo ni pamoja Umaskini, Migogoro ya familia, kuvunjika kwa ndoa, vifo vya wazazi au walezi lakini ipo sababu nyingine ambayo watu hawaitaji sana Umasikini, hivi vinachangia kwa kiasi kikubwa sana, umaskini ni sababu kubwa zaidi kwani wapo watu wanazaa wanashindwa kuwahudumia watoto na kuwaacha wakizurura mitaani”. amesema Mwasa.

Katika hatua nyingine Mwasa ameshauri Jukwaa la Kitaifa la Malezi Mbadala kuweka utaratibu utakao imarisha sera ya uzazi wa Mpango, kwani anaamini kuwa ongezeko la watu nchini limechagizwa na Wadau kupuuza uzazi wa mpango katika siku za hivi karibuni.

“Ongezeko la watu linakua kwa kasi sana ambapo takwimu za Sensa zinasema ongezekonni asilimia 3.5 kwa mwaka lakini kundi rika la miaka 8 kushuka chini lineongezeka sana,hii ni kwasababu kuna wakati suala la uzazi wa mpango lilisitishwa, Matangazo na Afua za kuzidhibiti uzazi holela zilikua zimesitishwa, sasa mtu anapo zaa ama kuzalisha bila kuwa na mipango watoto lazima wakose malezi na kuishia Mitaani” Amesema Mwasa.

Kuhusu hali ya Ukatili Nchini Mkuu wa Mkoa Mwasa amesema, Serikali inatambua mchango wa Wadau wote katika kusaidia kuchukua hatua dhidi ya ukatili.

“Ukatili upo kwa kasi, Serikali na Asasi za Kiraiya zimeendelea kupaza Sauti dhidi ya Ukatili hivyo kila Mwanajamii mmoja mmoja wanakuwa Mastari wa Mbele”

Mwasa ameliomba Jukwaa la Kitaifa la Malezi Mbadala kuendelea kuhamsisha jamii ili kuona umuhimu na kuwa na utayari wa kuwalea watoto wanaojikuta katika madhila hayo, Kwani inaumiza sana kuona Yatima anaenda kulelewa katika vituo vya yatima , Nyumba salama wakati wapo ndugu zake wenye uwezo wa kuwalea.

Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Ustawi wa jamii Baraka Makona amesema wameamua kuja na kitabu chenye kurasa kumi na tano zenye miongozo na maadili yanayotakiwa kufuatwa na watoa huduma kwenye sekta zote ili kuondoa wimbi kubwa la ukatili dhidi ya watoto Nchini.

“Kupitia kikao kazi hiki kuna maoni mengi sana tumeyapata kwa hiyo tumetengeza mpango kazi kwa maana ya Maazimio” amesema Makona

Awali akitoa salamu za Jukwaa kwa Mgeni Rasmi Mwenyekiti wa Jukwaa la Kitaifa la Malezi Mbadala Bi Ziada Nkinda amesema Jukwaa la Kitaifa la Malezi Mbadala limepokea maelekezo ambayo wizara imewapatia ili kuleta matokeo chanya ya Malezi Mbadala ya watoto wetu.