Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara
MKUU wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi,amewaagiza Maofisa Kilimo wote Mkoani humo kuhakikisha wanapeleka elimu ya Kilimo mseto na uhifadhi wa mazingira katika maeneo wanayofanyia kazi ili wananchi wazalishe mavuno yao kwa tija.
Kanali Mtambi ameyasema hayo Novemba 16, 2024 wakati akifunga maonesho ya tisa ya Kilimo mseto yaliyofanyika kuanzia Novemba 14, 2024, hadi Novemba 16, 2024, katika kituo cha mafunzo ya Kilimo mseto kilichopo kata ya Bweri Manispaa ya Musoma.
Amesema,kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, wakulima wanalojukumu la kuhakikisha wanalima Kilimo mseto kwa kutumia eneo dogo lakini wazalishe mavuno mengi na kutunza mazingira.Hivyo ili Jambo hilo lifanikiwe Maofisa Kilimo wanapaswa wawajibike kutoa elimu kwa wakulima.
“Maofisa Kilimo pelekeni elimu kwa wananchi walime Kilimo mseto na pia watunze mazingira yao ikiwemo uoto wa asili kwa kupanda miti kwa wingi. Ili tukabiliane na mabadiliko ya tabia nchi Kilimo mseto lazime kichukue nafasi kikamilifu. Pia kina tija kubwa sana katika kuzalisha chakula Cha kutosha. lazima wakulima wafanye Kilimo hiki, badala ya kulima kwa mazoea eneo kubwa mavuno kidogo.”amesema Kanali Mtambi.
Pia,Kanali Mtambi amelipongeza Shirika la Vi-Agroforestry kwa kuendelea kuwa Mdau muhimu wa uhifadhi wa Mazingira Mkoani humo na utoaji wa elimu bora ya Kilimo kwa wakulima katika kupambana na umaskini Jambo ambalo amesema limeendelea kuleta mageuzi na tija kwa wakulima.
Kwa upande wake Mratibu wa maonesho ya Kilimo Mseto Khalid Ngasa amesema Shirika la Vi-Agroforestry ni Shirika la Kiswidishi linalotekeleza miradi ya maendeleo nchini Tanzania tangu mwaka 1992. Na linaongozwa na mpango Mkakati wa miaka mitano ulioanza mwaka 2023 -2027 unaolenga kupambana na umaskini, mabadiliko ya tabia nchi.
Ngasa amesema,lengo la maonesho hayo ni kueneza ujumbe kuhusu mchango wa Kilimo mseto katika kuboresha matumizi bora ya ardhi, kuongeza pato la Mkulima na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Maonesho hayo amesema yamehudhuriwa na washiriki zaidi ya 3,600 kutoka serikali kuu, Watumishi ngazi yaMkoa, Wilaya, vyuo, taasisi za fedha na wakulima. Huku akisema shirika hilo limekuwa likishirikiana na Serikali, taasisi za umma, na mashirika yasiyokuwa ya Serikali ya ndani na Nje ya Nchini.
“kwa mwaka huu maonesho haya yameendana sambamba na uzinduzi wa mpango Mkakati wa Shirika la. Vi-Agroforestry (country strategy 2023-2027) pamoja na usambazaji wa Mpango wa pili wa Mkakati wa Kilimo mseto nchini ( 2024-2030) uliozinduliwa na Makamu wa Rais Dkt. Philipo Mpango katika maadhimisho ya siku ya misitu duniani machi 21, 2024.”amesema Ngasa.
Katika maonesaho hayo elimu ya uzalishaji mazao, uvunaji, uhifadhi,na uongezaji wa thamani wa mazao mbalimbali, zana bora za kilimo elimu ya lishe bora imeweza kutolewa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bunda Dkt. Vincent Naano amesema, wafugaji wengi wa Mkoa wa Mara wamekuwa wakichoma moto mbolea za mifugo yao, badala ya kaiweka katika mashamba yao kurutubisha ardhi Jambo ambalo pia limekuwa likichangia mavuno duni.
Akizindua maonesho hayo Novemba 14, 2024 , Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dunstan Kitandula alisema kuwa, serikali inalenga ifikapo mwaka 2030 kaya Mil. 15 ziwe zinatumia Kilimo mseto hapa nchini.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam