Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online, Shinyanga
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme amepiga marufuku tabia ya baadhi ya maofisa watendaji wa vijiji, mitaa na kata kuchati na simu wakati wakiwahudumia wananchi katika ofisi zao.
Mndeme ametoa tamko hilo wakati akizungumza na maofisa watendaji ngazi ya vijiji hadi kata kutoka wilaya za Shinyanga na Kishapu kwenye kikao kazi cha kupeana maelekezo ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika maeneo yao.
Mkuu huyo amesema kitendo cha baadhi ya watendaji kuwahudumia wananchi huku wakichati na simu kinaonesha dharau ya wazi mbele ya mwananchi anayehudumiwa na kwamba kuanzia hivi sasa tabia hiyo iachwe mara moja.
Amewataka watendaji hao waache milango wazi kwa wananchi ili kila pale wanapohitaji kuhudumiwa wahudumiwe kikamilifu kwa kusikilizwa kwa kina badala ya kusikilizwa huku mtendaji akichati na simu yake ya kiganjani.
Akifafanua amesema iwapo mtendaji itabidi kuongea na simu wakati akimhudumia mwananchi basi iwe ni simu ambayo inahusu suala la mwananchi huyo na ahakikishe awe amemtaarifu kwamba simu anayopiga inahusu suala lake.
“Nendeni mkatatue kero za wananchi huko kwenye maeneo yenu, na nitahitaji kupata taarifa kila mwezi ya jinsi mlivyoshughulikia kero za wananchi katika meneo yenu, eleweni moja ya majukumu na wajibu wenu ni kuwasaidia wananchi kutatua kero zinazowakabili,”
“Sambamba na hilo niwaombe watendaji, mnapofikiwa na wananchi wenye shida, acheni kuwasikiliza mkiwa mnachati na simu, elewa unapomuhudumia mwananchi huku unachati na simu ataona kama unamdharau, sasa nasema acheni kabisa, ikibidi kutumia simu kwa shida yake mfahamishe,” ameeleza Mndeme.
Amewataka watendaji hao wafahamu kuwa wananchi ndiyo kipaumbele chao hivyo wanapokwenda katika ofisi zao wasikilizwe kwa kina badala kuwasikiliza simu zikiwa mikononi wakichati na kwamba ye yote anatakayeendelea na mtindo huo atakuwa amekiuka maelekezo yake.
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa amewataka watendaji wote wa ngazi za vijiji na kata wajieupushe na tabia ya kupokea hongo kutoka kwa baadhi ya wazazi ama walezi ili kuruhusu kuwaozesha watoto wao walio chini ya umri wa miaka 18 ama wanafunzi.
Alielezea kushangazwa kwa kuona yeye binafsi anakwenda kijijini kuzuia ndoa za watoto wenye umri mdogo ambazo zilikuwa zikifungwa huku maofisa watendaji na viongozi wengine wa kiserikali wakiwa wamefumbia macho kitendo hicho.
“Nendeni mkasimamie suala la vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikiwemo ndoa za utotoni na mchukue hatua stahiki dhidi ya wale wote wanaofanya ukatili kwenye jamii, iwe wa watoto au ukatili wa baba na mama, kasimamieni kwa vitendo, haiwezekani mtendaji wa kata upo ukatili ufanyike,”
“Nina taarifa baadhi ya watendaji wa vijiji, mitaa na kata siyo waaminifu mnapokea hongo na kuruhusu ndoa za utotoni, mnapewa ng’ombe, mbuzi ama pesa mnaruhusu mtoto anaozeshwa, hii haiwezekani, yaani mpaka mimi mkuu wa mkoa ninakwenda kuzuia ndoa hiyo wewe mtendaji upo, hapana,” ameeleza Mndeme.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi