November 9, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rc Mbeya aagiza kusakwa kwa watu wenye ulemavu nyumba kwa nyumba

Na Esther Macha,Timesmajira Online, Mbeya

SERIKALI mkoani Mbeya imewaagiza maafisa maendeleo ya jamii wa wilaya zote mkoani hapa kupita nyumba kwa nyumba  kusaka watu wenye ulemavu ili waweze kupatiwa mikopo ya asilimia 10  ambayo hutolewa na halmashauri kwa ajili ya   vikundi vya vijana ,wanawake na walemavu.

Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa mkoa wa mbeya ,Juma Homera wakati wa kikao cha kujibu hoja  za mkaguzi wa hesabu za serikali  kwa mwaka 2021/2022 kwa halmashauri ya wilaya ya Kyela.

Aidha Homera amesema kuwa kila halmashauri ihakikishe inawatafuta wenye ulemavu nyumba kwa nyumba ili waweze kupatiwa mikopo .

Hata hivyo Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa asilimia 40 inayotengwa kwa ajili   ya miradi ya maendeleo ipelekwe kikamilifu  na asilimia 10 inayokwenda kwa kwa vikundi vya wanawake ,vijana na watu wenye ulemavu iende kwa walengwa wenyewe.

“Maafisa maendeleo ya jamii  wilaya tafuteni  hata mmoja mmoja  watu wenye ulemavu sio lazima wawe sita wengi mtawapata wapi hao wengine wanafichwa ndani ,hii nayo ni hoja  kwa mdhibiti  mkuu wa hesabu za serikali maana kila mara tumekuwa tukiulizwa kwanini  walemavu idadi yao kwenye vikundi ni ndogo sana kulinganisha na fedha zinazotengwa ,nakuagiza ofisa maendeleo ya jamii wilaya kusaka nyumba kwa nyumba wati wote wenye ulemavu “amesema Homera.

Hata hivyo Homera amesema kuwa maafisa maendeleo ya jamii washirikiane na wenyeviti wa vijiji ,mabarozi katika kuwasaka watu wenye ulemavu ,walemavu wasakwe hiyo ndo itakuwa salama ya mkoa wa Mbeya.

“Tunataka mikopo  ijayo mh.Mkuu wa wilaya na mwenyekiti wa halmashauri  hakuna kwenda kugawa mikopo pasipo  kuwepo kwa vikundi vya  watu wenye ulemavu ,hatuwezi  kukubali kwenda hivi bila  kujali  watu wenye ulemavu “amesema mkuu wa mkoa wa Mbeya.

Kwa upande wake mkazi wa Kyela mkoani  Mbeya Asifiwe George ameshauri serikali kufika maeneo ya vijijini ambako ndiko kuna walemavu wenye uhitaji wa mikopo.

Aidha amesema kuwa kikubwa kinachotakiwa ni kuwapa elimu ya mikopo tu hakuna ambaye atashindwa kufanya marejesho vizuri.