January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Makalla: Tanzania tuna mafuta ya kutosha kutumia mpaka July 15

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla amesema kiasi cha akiba ya nishati ya mafuta kilichopo Sasa na yale yaliyopo kwenye Meli yakishushwa yatatosha kutufikisha mpaka July 15 mwaka huu hivyo hakuna sababu yoyote ya Wananchi kuwa na hofu.

Hayo ameyasema leo jijini Dar es salaam alipokutana Na wadau wa mafuta Na wakala wa uagizaji mafuta pamoja kwa lengo la kutoa mrejesho wa kamati ya uchunguzi wa wizi wa mafuta Na kupokea taarifa ya hali ya mafuta nchini.

Aidha RC Makalla amesema kiasi Cha Mafuta yaliyopo Sasa ukijumlisha na Yale yatakayoshushwa na Meli yatafanya Nchi kuwa na akiba ya Lita Milioni 512.7 za Dizeli, Petrol Lita Milioni 365.5, Mafuta ya ndege Lita Milioni 40 na Mafuta ya taa Lita Milioni 5.9 ambapo kwa pamoja yanaweza kutumika mpaka July 15 mwaka huu.

Kutokana na Mkoa wa Dar es salaam kuwa lango kuu la Biashara ya mafuta, RC Makalla amesema Serikali itaendelea kulinda na kudhibiti Miundombinu ya Mafuta ili kutokomeza tatizo la Wizi na uchepushaji wa Mafuta na usalama wa Wananchi ambapo amesema kwa Sasa Bomba la Mafuta lipo salama.

Hata hivyo RC Makalla ametoa Matokeo ya Kamati aliyounda kuchunguza Wizi wa Mafuta kutoka bomba kuu ambapo amesema zaidi ya watu 15 walikamatwa na wapo Chini ya Vyombo vya sheria na kueleza kuwa tayari Serikali imefanyia kazi mapendekezo ya Kamati ikiwa ni pamoja na kufukua upya Bomba la Mafuta na kulifukia na ununuzi wa kifaa Cha kutambua wapi Bomba limechepushwa.

Kuhusu suala la foleni za malori Bandarini zinazosababishwa na upanuzi wa Barabara, RC Makalla ameelekeza Shughuli za Ujenzi kufanyika pasipokuathiri Shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja Ujenzi barabara ya kuingia Na kutoka bandarini kufanyika usiku.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wakala wa uagizaji Mafuta kwa pamoja Erasto Simon na Wadau wa Mafuta kwa pamoja wamemshukuru RC Makalla kwa hatua za haraka alizochukuwa kudhibiti tatizo la Wizi na uchepushaji wa Mafuta lililokuwa limedumu kwa muda mrefu na Sasa wanakiri kupokea kiasi Cha Mafuta sawa na kile walichoagiza.