December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Kunenge: Usahihi wa taarifa za Jeshi kuhusu ajali zinazowafikia wafanyakazi ni muhimu kwa malipo ya fidia

 Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Alhaj. Aboubakar Kunenge, amesema, utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), hususan katika kulipa fidia kwa mfanyakazi aliyeumia au kufariki kutokana na ajali utatekegemea sana usahihi wa taarifa za Jeshi la Polisi.

Mhe. Alhaji Kunenge ameyasema hayo Septemba 26, 2023, wakati akifungua kikao kazi baina ya WCF na Makamanda wa Polisi wa Usalama Barabarani wa Wilaya (DTOs)na Wakaguzi wa Polisi wa Usalama Barabarani wa Wilaya za Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, kilichofanyika mjini Kibaha.

“Kuna wadau mbalimbali katika mnyororo wa WCF katika kuwahudumia wananchi na miongoni mwa wadau hao ni Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani.” Alisema.

Alisema kwa mujibu utaratibu wa utoaji taarifa kwa mfanyakazi aliyepata ajali ya barabarani, Jeshi la polisi ndio lenye mamlaka ya kisheria kuthibitisha uwepo wa ajali na kwamba taarifa hiyo ndiyo itatoa muongozo wa uchakataji wa madai kabla ya muhusika kulipwa fidia.

Alisema endapo Jeshi la Polisi halitafanya yale ambayo linapaswa kufanya katika kuthibitisha ajali, mchakato mzima utakuwa umeharibika na kunakuwepo na uwezekano wa kulipa fidia kwa mtu ambaye hastahili kulipwa na hivyo kupelekea upotevu wa fedha za umma.

Akimkaribisha mgeni rasmi kufungua kikao kazi hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini WCF, Bw. Emmanuel Humba, alisema, WCF iliingia makubaliano ya ushirikiano na Jeshi la Polisi ili kurahisisha utoaji huduma kwa wnaanchi na hasa kuwezesha haki kutendeka bila ya kuumiza upande wowote.

“Malipo ya fidia hayawezi kufanyika bilaya  taarifa sahihi kutoka Jeshi la Polisi inapotokea ajali iliyomuhusisha mfanyakazi akiwa anatekeleza majukumu ya mwajiri wake kwa mujibu wa mkataba wa ajira.” Alifafanua Bw. Humba.

Aidha Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini SACP. Ramadhani Ng’anzi amewasisitizia Polisi wa Usalama Barabarani kuzingatia kanuni za kudumu za Jeshi la Polisi, (Police General Order (PGO). Alisema, taarifa ya Jeshi la Polisi lazima ieleze uhalisia wa tukio na si vinginevyo.

“Kwanafasi yako ukiwa kama afisa wa polisi uadilifun ni jambo muhimu sana, nimesema uwe ofisini au nje ya ofisi wananchi wameweka imani kubwa sana kwetu.” Alifafanua.

Kwa upandew wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZTO), Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP. William Mkonda alisema, Makamanda wa Kikosi cha Usama Barabarani wa Wilaya (DTOs) ni lazima wajenge tabia ya kudodosa taarifa wanazopelekewa na askari wanaowaongoza.

“Tuwe makini, tusome nyaraka zetu kabla hatujasaini, lakini huduma hizi tuzitoe kwa wakati, PF90 inatumia wiki nzima mwananchi kuifuata kituo cha polisi? alihoji ACP Mkonda na kusisitiza kuwa lazima huduma hiyo itolewe kwa haraka ili haki iweze kutendeka.

Kwa mujibu wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Mfanyakazi aliyeumia kutokana na ajali anapaswa kutoa taarifa kwenye Mfuko, ndani ya miezi 12 tangu tukio hilo litokee akiwa na taarifa ya polisi inayothibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Alhaj. Aboubakar Kunenge, akizungumza kwenye kikao akzi hicho.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini WCF, Bw. Emmanuel Humba, akitoa nasaha zake mwanzoni mwa kikao hicho.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, SACP. Ramadhani Ng’anzi, akizunhuzma na makamanda hao

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaji Aboubakar Kunenge (kushoto), akifurahia jambo na Mwenyekiti wa Bodia ya Wadhamini Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Emmanuel Humba, (wapili kushoto), Mkurugenzi Mkuu, WCF, Dkt. John Mduma, (watatu kushoto), Mkuu wa Polisi wa Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Mwandamizi wa Polisi, SACP. Ramadhani Ng’anzi (wakwanza kulia) na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP. William Mkonda, baada ya ufunguzi wa kikao kazi baina ya Mfuko na Makamanda wa polisi wa Usalama Barabarani wa Wilaya za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na Wakaguzi wa Polisi kutoka mikoa hiyo. Kikao hicho kimefanyika Kibaha, Septemba 26, 2023.

Baadhi ya makamanda wakifuatilia mafunzo hayo

Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP. William Mkonda, akifafanua jambo wakati akitoa nasaha zake kwa makamanda hao

Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Deus Sokoni, akitoa mada kuhusu umuhimu wa kuandika taarifa sahihi kwa ajili ya kuchakata madai ya fidia.