Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MKUU wa Mkoa wa Tabora Ali Salum Hapi amewataka Wakurugenzi Watendaji wa halmashauri 8 za mkoa huo kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato na kuhakikisha kila mmoja anafikia lengo lililowekwa katika halmashauri yake.
Ametoa onyo hilo juzi alipokuwa akiongea na Viongozi, Watendaji na wawakilishi wa wananchi katika hafla ya makabidhiano ya Ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Dkt Philemon Sengati ambaye amehamishiwa Mkoa wa Shinyanga.
Amesema mkoa huo umejaaliwa kuwa na rasilimali na vyanzo vingi vya mapato hivyo akawataka Wakurugenzi, Wataalamu na Watendaji walioko katika halmashauri hizo kusimamia ipasavyo ukusanyaji mapato na kubuni vyanzo vipya.
Ameongeza kuwa mkoa huo wenye takribani watu mil 3 umejaaliwa pia kuwa na ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali na mifugo mingi lakini bado haufanya vizuri hivyo akawataka kuongeza juhudi zaidi ya usimamizi.
“Kama niliweza kukusanya sh bil 20 za mapato katika Mkoa wa Iringa ambao ni mdogo kwa nini Tabora ishindwe, nataka tuongeze juhudi na kasi zaidi ili kuongeza mapato’, amesema.
Hapi amebainisha kuwa taarifa inaonyesha hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu Mkoa huo ulikuwa umekusanya asilimia 59 tu na umebaki mwezi 1 kumaliza mwaka wa fedha, hivyo akaagiza kila halmashauri kuhakikisha inafikia malengo.
Aidha amewataka Viongozi na Watumishi wa halmashauri zote za Mkoa huo kushikamana na kuchapa kazi kwa bidii huku akiwataka kujiepusha na tabia za majungu kwa kuwa hayajengi, bali hurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.
Amesisitiza kuwa dhamira yake ni moja tu ya kuwaleta maendeleo wananchi hivyo akaagiza kila kiongozi kutenda haki, kuwa mkweli na kuwajibika ipasavyo katika eneo lake au idara yake ikiwemo kutembelea wananchi ili kuleta matokeo chanya.
Aidha amebainisha kuwa atahakikisha huduma za jamii zinaboreshwa kwa kiasi kikubwa katika maeneo yote na hatamvumilia mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na wizi wa dawa au vitendo vyovyote vya ubadhirifu.
Mkuu huyo ameagiza watumishi kwenda kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi ili kupunguza mlundikano wa mashauri yanayopelekwa mahakamani kwani mengi husababishwa na viongozi kutokuwa karibu na jamii.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea