Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MKUU wa Mkoa wa Tabora ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo Paul Matiko Chacha amewahakikishia wakazi wa Mkoa huo ulinzi wa kutosha usiku na mchana baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo.
Ameeleza hayo jana alipokuwa akizungumza na Mashehe wa Wilaya zote za Mkoa huo, viongozi wa madhehebu ya dini, wadau mbalimbali na waumini wa dini ya kiislamu katika hafla maalumu aliyoandaa ili kujitambulisha na kula futari pamoja.
Amebainisha kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amemteua ili kuwatumikia wakazi wa Mkoa huo kwa niaba yake hivyo akawahakikishia kuwa atawatumikia kwa moyo wa dhati na Ofisi yake iko wazi wakati wote kusikiliza shida zao.
RC Chacha amesisitiza kuwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa ni Ofisi ya umma hivyo wananchi wana haki ya kuja wakati wowote wanapokuwa na kero au hata kuja kumsalimia tu Kiongozi wao, vivyo hivyo kwa Ofisi za Wakuu wa Wilaya.
‘Ndugu zangu nimewaiteni hapa ili kuwashukuru kwa kunipokea vizuri, ombi langu kubwa kwenu ni ushirikiano, jukumu langu kubwa ni kuhakikisha mnalala salama na kuamka mkiwa salama ikiwemo kulinda utu na haki zenu’, amesema.
Ameongeza kuwa ameandaa hafla hiyo ili wakutane na kula futari pamoja na kujitambulisha rasmi kwao baada ya kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mkuu mpya wa Mkoa huo akitokea Wilaya ya Misungwi alikokuwa Mkuu wa Wilaya.
Awali Shekhe Mkuu wa Mkoa huo Shekhe Ibrahim Mavumbi amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuandaa iftar hiyo na kuwaalika mashekhe, viongozi mbalimbali na waumini wa dini ya kiislamu katika mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
‘Kuwafuturisha waislamu na wasio waislamu katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan ni ibada inayompendeza Mtume wetu Mohammad SA na Mwenyezi Mungu, tunakushukuru sana na tunaahidi kukupa ushirikiano wa kutosha’, amesema.
Ameomba waislamu wote kushiriki ibada ya sala ya idd itakayofanyika katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi na Baraza la Idd litakalofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma mjini hapa mwezi utakapoandama.
Akitoa salamu kwa niaba ya Maaskofu, Askofu Dkt Elias Chakupewa wa Kanisa la Anglikana Mkoani hapa amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa moyo wake wa upendo na kuwatakia heri na baraka tele waislamu wote waliopo katika mfungo.
More Stories
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake