Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
SERIKALI Mkoani Tabora imetoa onyo kali kwa wanaume wenye tabia ya kulaghai watoto wa shule za msingi na sekondari kwa lengo la kufanya nao mapenzi na kubainisha kuwa kiama chao kimefika.
Onyo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chacha alipokuwa akiongea na walimu na wanafunzi wa shule za msingi kutoka Mikoa 28 ya Tanzania Bara na Visiwani wanaoshiriki UMITASHUMTA Mjini hapa.
Amesema kuwa serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira bora katika shule zote ili kuwezesha watoto wote kupata elimu, hivyo akaonya wanaume wanaokatisha ndoto za mtoto wa kike.
Amesisitiza kuwa yeye kama Mkuu wa Mkoa huo atahakikisha watoto wote wa kiume na kike wanalindwa na kupatiwa haki zao za msingi ikiwemo elimu na kuongeza kuwa mafataki wote wanaorubuni watoto wa kike watakiona cha moto.
‘Yeyote atakayemchezea mtoto wa kike, kumwoa au kumtia mimba, akajisalimishe mwenyewe Kituo cha Polisi hata hata kabla sijamkamata, katika hili sitapepesa macho, sheria itachukua mkondo wake’, amesema.
RC Chacha amepongeza kazi nzuri inayoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya 6 katika Mkoa huo kwani katika kipindi cha miaka 3 tu wameshapokea zaidi ya sh bil 260 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo katika sekta ya elimu.
Amefafanua kuwa sh bil 144 zimetumika kuboresha miundombinu ya elimu na michezo, sh bil 103 zimetumika kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari na sh bil 41 zimegharama elimu bila maalipo.
Aidha Chacha amemshukuru Mhesh.Rais kwa kuwaletea kiasi cha sh bil 3.4 kwa ajili ya kuzifanyia ukarabati mkubwa shule 4 kongwe za Mkoa huo ambazo ni shule ya sekondari ya Tabora Wavulana, Tabora Wasichana, Milambo na Kazima.
Kutokana na mvua kubwa zilizonyesha mwaka huu Chacha ameeleza kuwa wanatarajia kuvuna kilo mil 114 za tumbaku ambazo zitawapatia kiasi cha sh bil 17, na kusisitiza kuwa wataendelea kulinda miti na kuzuia uharibifu wa mazingira.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua