November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Batilda azindua ujenzi mabwawa ya kutibu majitaka

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoani Tabora (TUWASA) imezindua mradi wa ujenzi wa Mabwawa ya kutibu majitaka yanayokusanywa na magari/maboza kutoka katika makazi ya wananchi na maeneo ya biashara.

Mradi huo wa ujenzi wa mabwawa makubwa utatekelezwa katika halmashauri ya manispaa Tabora na Mkandarasi Peritus Exim Private Limited ya Jijini Dar es salaam kwa gharama ya sh bil 1.6 na unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 12.

Akizindua mradi huo jana Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya majisafi na salama.

Alisema ujio wa mradi huo ni habari njema kwa wakazi wa manispaa hiyo na Mkoa mzima kwani utasaidia kuboresha afya za wananchi na kuchochea maendeleo makubwa ya manispaa hiyo na hatimaye kuifanya kuwa jiji.

Alipongeza utendaji wa Mamlaka zote mbili TUWASA na RUWASA kwa kufanya kazi nzuri ambayo imepelekea kuongeza kiwango cha upatikanaji huduma ya maji mjini na vijijini na kusaidia wananchi wasiojiweza kupata huduma hiyo.

Balozi Batilda aliwataka Viongozi wa Mamlaka hiyo kusimamia kwa dhati mradi huo ili utekelezwe kwa kiwango kinachotakiwa na thamani ya fedha iendane na kazi itakayofayika na kukamilisha mradi huo kwa wakati.

Akiongea katika hafla hiyo kwa niaba ya Waziri wa Maji, Mhandisi Mkuu wa Wizara hiyo Loishiye Ngotee alisema miradi hiyo inatekelezwa katika Miji 10 hapa nchini ikiwemo Mji wa Tabora.                                                                                                                         

Alitaja miji mingine 9 kuwa ni Kahama, Kigoma, Sumbawanga, Mpanda, Lindi, Mtwara, Njombe, Geita na Singida.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo kabla ya kusaini mkataba wa kuanza ujenzi, Mkurugenzi Mtendaji wa TUWASA, Mhandisi Mayunga Kashilimu alisema serikali kupitia Wizara ya Maji imewapa kibali cha kujenga mabwawa hayo.

Alisema yatajengwa eneo la Milambo Barracks pembezoni mwa mabwawa ya zamani yanayohifadhi majitaka ambayo hayana uwezo wa kutibu maji hayo, aliongeza kuwa maji hayo yakitibiwa yatakuwa tayari kwa matumizi mengine ikiwemo kilimo cha umwagiliaji.

Alimshukuru Rais Samia kwa kuwapatia kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kujenga mabwawa hayo yanayopokea maji machafu kutoka kwenye makazi ya watu na sehemu za biashara ambapo asilimia 91.6  ya wakazi wa manispaa hiyo hutumia vyoo vya shimo ambavyo kuzalisha lita mil 15.6 za majitaka kwa siku.

Mhandisi Mayunga alitaja baadhi ya faida za mradi huo kuwa ni kuboresha usafi wa mazingira na afya kwa wakazi wa manispaa hiyo, kutumia maji hayo kwa shughuli za kilimo cha mbogamboga (umwagiliaji) na kutoa ajira kwa jamii.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni inayotekeleza mradi huo, Triporari Goyal alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa atafanya kazi kwa weledi mkubwa na atamaliza kazi hiyo kwa muda uliopangwa.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora Elias Mpanda alisema mradi huo ni utekelezaji ilani ya uchaguzi ya chama hivyo Mkandarasi anapaswa kutumia sh bil 1.6 zilizoletwa na serikali kwa manufaa ya wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian (mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali wa chama na serikali na Watumishi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira ((TUWASA) baada ya kuzindua ujenzi wa mradi wa mabwawa ya kutibu majitaka utakaotekelewa katika halmashauri ya manispaa tabora kwa gharama ya sh bil 1.6. Pichana Allan Vicent.