Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
WAKULIMA wa zao la tumbaku Wilayani Sikonge Mkoani Tabora wametakiwa kujiepusha na vitendo vya utoroshaji au uuzaji zao hilo kinyume na utaratibu katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye msimu mpya wa masoko.
Onyo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alipokuwa akiongea na Viongozi wa vyama vya msingi, Wataalamu na Maofisa mbalimbali wa serikali katika ukumbi wa Mwanambuya Wilayani Sikonge.
Alisema serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeweka utaratibu mzuri ili kuhakikisha tumbaku yote itakayolimwa msimu huu inanunuliwa kwa bei nzuri iliyoelekezwa ili kumnufaisha mkulima.
Alisisitiza kuwa katika msimu huu makampuni makubwa ya ndani na nje yamejitokeza kwa ajili ya kununua tumbaku yote itakayozalishwa na wakulima kupitia vyama vyao vya msingi, hivyo haina haja ya kwenda kuuza kimaficho.
‘Ni marufuku kwa mkulima yeyote kutorosha au kwenda kuuza tumbaku yake nje ya utaratibu uliowekwa, atakayebainika kwenda kinyume atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria,’ alisema,
Balozi Batilda aliwataka kuzingatia kanuni, taratibu na malekezo ya watalamu ili kulima kwa tija na kuongeza uzalishaji wa zao hilo, na kubainisha kuwa mwaka jana pekee jumla ya kilo mil 30 za tumbaku zilizalishwa na mwaka huu wamekisia kuzalisha kilo mil 60.
Akiongea kwa niaba ya wakulima, Katibu Meneja wa chama cha msingi Tumaini, kata ya Mole, Paul Maziku alisema utoroshaji tumbaku huchangiwa na wanunuzi kuchelewesha sana malipo ya wakulima, wakibadilika hakuna atakayetorosha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku (WETCU LTD) Hamza Kitunga alisema serikali ina dhamira ya dhati ya kuboresha shughuli za wakulima na kumaliza changamoto zinazowakabili.
Alisisitiza kuwa mwaka huu hawatakubaliana na kampuni yoyote itakayokuja na hadithi ya zamani ya kutaka kununua tumbaku ya wakulima kwa mkopo, na kubainisha wazi kuwa kila mnunuzi atalipa fedha taslimu.
Meneja Mkuu wa WETCU Samwel Jokeya alisema katika kipindi cha miaka 3 uzalishaji wa zao hilo umeendelea kuongezeka maradufu katika Mkoa huo hivyo kuwezesha wakulima kuendelea kunufaika.
Alibainisha kuwa athari za ulanguzi na utoroshaji zao hilo bado ni kubwa kutokana na baadhi ya wakulima kutokuwa waaminifu, hivyo kupelekea mapato mengi ya wakulima kupotea, alishauri kila mkulima kujiunga na chama cha msingi.
More Stories
Wanafunzi 3000 wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Rais Samia, Mwinyi ‘mitano tena’ Nchimbi aula
Dkt.Kikwete:Ushindi wa CCM ni lazima