January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC akerwa na watendaji kushindwa kutatua kero za wananchi.

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

MKUU wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amekerwa na baadhi ya watendaji kushindwa kutatua kero za wananchi kwa wakati hali inayowalazimu kuwatafuta Viongozi wa ngazi za juu ikiwemo Ikulu.

Kufuataia hali hiyo, Mrindoko amewataka viongozi wote mkoani humo kujiwekea utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi na baada ya hapo apate ripoti ya hali ya migogoro na utatuzi wake kila baada ya Mwezi ili kumsaidia Rais kutatua changamoto zilizo ndani ya uwezo wao kabla hazijamfikia.

Akizungumza katika kikao kazi na Watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa kilichofanyika Jana Januari 20,2023 katika Ukumbi wa Mpanda Mancipal Social Hall RC Mrindoko amesema viongozi hao kushindwa kuwa karibu na wananchi kumepekelea baadhi ya kero zilizotakiwa kutatuliwa ngazi ya Mtaa, Kijiji, Kata au halmshauri kufikishwa kwa viongozi wa TAMISEMI hadi Ikulu jambo ambalo hajapendezwa nalo.

“Nisisitize, kila mmoja ahakikishe kero zinazotatulika kwenye levo yake azitatue kikamilifu na ukishazitatua umpe majibu mlalamikaji na mlalamikiwa pamoja na mamlaka nyingine zinazohusika kwa sababu zitaturahisishia kwamba mgogoro flani umeshatatuliwa kwa njia hii na sasa tutalitazama utatuzi wake kama bado unalalamikiwa ulikuwa halali au sio halali na tutaona hatua nzuri za kuchukua ili kumaliza jambo hilo “

Aidha, amewataka viongozi hao kuwa waadilifu kwa kutenda haki pale mwananchi anapofikisha lalamiko lake, kujiepusha na vitendo vya rushwa ili wananchi wawe na imani na uongozi wao hasa kunapotolewa suluhu la jambo flani.

“Niwatake kuhakikisha msiwe chanzo cha kuzalisha kero mpya, msiwe chanzo cha kuzusha migogoro kati ya watumiaji wa Ardhi na hasa kwenye eneo hili kuna baadhi ya Viongozi wasio waaminifu wanatuvuruga,badala ya kufanya uongozi wa kutatua matatizo, kero na changamoto wanakuwa ni mwanao wa kuzalisha migogoro”

RC Mrindoko amesema Serikali haitamvumilia kiongozi yeyote atakayekuwa chanzo cha kuzalisha migogoro mipya hasa kiongozi kushiriki kupima maeneo ambayo fika anajua ni yawazi au eneo moja kuuzwa zaidi ya mara mbili huku yeye akiwa shuhuda kiongozi huyo atachukuliwa hatua za kisheria.

Amewataka kabla ya kufanya uamuzi wowote, wajiridhishe kwanza na eneo husika kwa kuwasiliana na uongozi wa juu.

“Wananchi wetu wanatupa taarifa, kama wewe Mtendaji hauko vizuri hata kama hawatasema mbele yako tuko kwenye mkutano tukiondoka watatutumia meseji, watatupigia simu jamani anayevuruga mambo yote ni Mtendaji wa mtaa, anayetuvurigia mambo yote hapa ni Mtendaji wetu wa kijiji. Naomba mkasimame kwa uadilifu unaostahili katika utumishi wa Umma”

Pia amewataka kuwa karibu na wananchi ili iwe vyepesi kwao kufikisha kero kwa wakati kabla hajachukua uamuzi wa kuwatafuta Viongozi wa ngazi za juu.