Na Albano Midelo,TimesMajira Online, Ruvuma
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amewakabidhi wakuu wa wilaya watano vipaza sauti kwa ajili ya utoaji wa elimu kwa jamii ya kujikinga na ugonjwa wa corona.
RC Ibuge amekabidhi vifaa hivyo katika hafla fupi iliyofanyika kwenye viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma mjini Songea.
Amewaagiza wakuu wa wilaya wanapokwenda kwenye maeneo yao ya kazi,kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika kuendelea kuwahamasisha wananchi kujikinga na kuchukua hatua zinazostahiki dhidi ya ugonjwa wa homa kali mapafu yaani UVICO 19.
Akizungumza baada ya kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,vifaa vya kutolea elimu dhidi ya corona,Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Dr.Jairy Kanga amesema Dunia hivi sasa ipo katika mapambano makali dhidi ya UVICO 19 hivyo elimu endelevu inatakiwa kutolewa kwa wananchi.
Ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya kuambukiza ikiwemo corona kwa kuvaa barokoa wanapokuwa kwenye mikusanyiko na ametoa rai kujiepusha na misongomano isiyokuwa ya lazima.
“Kila inavyowezekana tutumie vipukusa mikono (sanitizer),njia rahisi na salama zaidi kwa wananchi ni kunawa mikono kwa kutumia maji yanayotiririka kwa kutumia sabuni,naamini kila Mtanzania ana sabuni’’,amesisitiza.
Hata hivyo amelitaja jambo muhimu katika kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza ni kufanya mazoezi kwa sababu mazoezi yanaamsha kinga za mwili na kufanya mtu kuwa na kinga bora hivyo kuepukana na magonjwa ya kuambukiza.
Mganga Mkuu huyo wa Mkoa wa Ruvuma amesema kuna viashiria vya kuingia wimbi la tatu la corona hapa nchini ambapo tayari nchi jirani zetu kama Kenya wameingia kwenye wimbi la tatu,hivyo amesisitiza ni vema kuchukua tahadhari,ingawa amesema hadi sasa katika Mkoa wa Ruvuma hakuna mgonjwa wa Corona.
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM