Na Tiganya Vincent, TimesMajira online,Tabora
WAKUU wa Idara za Halamshauri za Wilaya, Mkoani Tabora wametakiwa kuondoka Ofisini ili kwenda kwa wananchi kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali zinazowakwaza kwenye juhudi zao za kujiletea maendeleo.
Agizo hilo limetolewa jana wilayani Urambo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Ally Hapi wakati wa mkutano na Watumishi wa umma kutoka Taasisi mbalimbali.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuondoa suala la wananchi kuandika mabango pindi viongozi wa Kitaifa wanapokuwa na ziara katika maeneo mbalimbali Mkoani humo.
“Mbinu ya kupunguza mabango kwa wananchi ni kuwatembelea wananachi kila mara kwa ajili ya kuzungumza nao na kusikiliza shida zao na kuzitafutia ufumbuzi…ndio maana mimi muda mwingi nautumia kusikiliza kero mbalimbali za wananchi badala ya kukaa ofisini” amesisitiza
Hapi amesema tatizo la kutokwenda kwa wananchi linasababisha wakati mwingine kuwafanya waichukie Serikali yao kwa sababu ya kukosa watu wa kusikiliza kero zao.
Amesema wananchi ndio walioiweka Serikali madarakani kwa hiyo wanapaswa kusikiliza na kutatualiwa matatizo yao.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Tabora ameagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo na Kaliua kuweka mpango wa kulipa madeni mbalimbali ya watumishi.
Amesema hatua hiyo itasaidia morali na moyo wa watumishi kufanyakazi kwa bidii bila manung’uniko na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Hapi ameongeza pamoja na Wakuu wa Idara kulipa madeni mbalimbali wazodaiwa na watumishi ni vema wakiwa na muda wa kusikiliza kero zao kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika utumishi wao.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi