Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto
KATIBU Tawala Mkoa wa Tanga Pili Mnyema ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kwa kuweza kuvuka lengo la makusanyo ya Mapato ya ndanni wa robo mbili za kwanza za mwaka wa fedha 2024/2025 kwa kukusanya sh. bilioni 1.5 sawa na asilimia 53.
Na kuongeza kuwa mapato hayo ikawe chachu ya kukusanya Mapato ya Ndani kwa asilimia 100 kwa halmashauri zote 11 za Mkoa wa Tanga, kwani kwa kuweza kukusanya mapato mengi, ndipo halmashauri hizo zitaweza kuhudumia wananchi kwa kujenga miradi ya maendeleo.
Hayo yamesemwa na Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Ramadhan Ally Januari 23, 2025 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto na kuongeza kuwa, pamoja na fedha hizo kutekeleza shughuli za maendeleo, pia waweze kujenga Ofisi za Watendaji wa vijiji na kata ili kurahisisha shughuli za maendeleo.
Ally ambaye ni Afisa Tawala Mwandamizi, Idara ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa, alisema halmashauri inapokusanya mapato ya ndani kwa ukamilifu, inawaaaidia wananchi wake kupata uhakika wa huduma za jamii.
“Katibu Tawala Mkoa wa Tanga anawapongeza Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kwa kuweza kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa robo mbili za kwanza. Na anawataka muweze kufanya vizuri kwenye makusanyo hayo ili muweze kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato hayo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
“Lakini pia katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, pamoja na kufanya shughuli nyingine za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi, pia mnatakiwa kujenga Ofisi za Kata na Vijiji. Ofisi hizo zitasaidia kuharakisha shughuli za maendeleo ya wananchi,”amesema Ally.
Ally amesema halmashauri hiyo yenye vijiji 134 na kata 34, inatakiwa kujenga Ofisi za Mtendaji wa kata 15 na Ofisi za Mtendaji wa vijiji 55.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mara baada ya kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Dkt. Ikupa Mwasyoge amesema pongezi za Katibu Tawala Mkoa wa Tanga wamezipokea, na watazifanyia kazi ili kuona wanafikia lengo la ukusanyaji mapato kwa zaidi ya asilimia 100 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
“Tumepokea pongezi kutoka kwa mwajiri wetu, Katibu Tawala alizozitoa kwa Mkurugenzi, Watumishi na Madiwani baada ya kuona kazi iliyofanyika. Ni kweli, bajeti tuliyotakiwa kuitekeleza ni ya sh. bilioni 2.9, lakini kufikia robo hii ya pili, tumeweza kukusanya sh. bilioni 1.5 sawa na asilimia 53, na bado tunaendelea kupambana ili kuhakikisha ile bajeti ambayo tumepewa kuweza kuifikia na Mungu akituwezesha kwenda kuzidi.
“Na hii imechangiwa sana na viongozi wetu kwa ushauri wanaotupatia, maelekezo na usimamizi na ufuatiliaji wao wa mara kwa mara unatufanya kuwa namna hii. Hivyo tunaendelea kushukuru viongozi wetu wa ngazi ya mkoa, wilaya na halmashauri kwa kazi wanayoifanya na ushirikiano wanaotupatia hata tunafikia malengo haya” amesema Dkt.Mwasyoge
Katika hatua nyingine Dkt.Mwasyoge amesema, halmashauri hiyo imegawa vishkwambi 65 vyenye thamani ya sh.17,225,000 kwa madiwani 45 na watumishi 20 ili viweze kuwasaidia kwenye shughuli za kila siku za halmashauri, kwani kwa madiwani kupata vishkwambi hivyo, pia watapata taarifa kwa wakati, huku ikipunguza gharama ya kuchapa makabrasha na kuyapeleka kwa gari makabrasha hayo kwa madiwani kwenye kata zao.
“Tumeweza kununua vishkwambi 65 vyenye thamani ya sh. 17,225,000 na kuwakabidhi madiwani 45 na watumishi 20. Vishkwambi hivi vina faida kubwa sana hasa nyakati hizi ambapo Serikali inahimiza Serikali Mtandao (eGovernment), kwamba taarifa ziwe zinatolewa kupitia eGovernment sababu kuna ufanisi mwingi na unafuu mwingi unapatikana kwa kutumia hii mifumo ya kimtandao,”amesema Dkt.Mwasyoge.
Hafla ya kukabidhi vishkwambi hivyo ilifanyika sambamba na kikao cha Baraza la Madiwani, ambapo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Mathew Mbaruku alikabidhi vishkwambi hivyo kwa madiwani.
More Stories
Kambi ya wanasheria Katavi kuwajengea uwezo wananchi
Serikali yaimarisha uchumi wa kidigitali kukuza biashara mitandaoni
Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu latakiwa kutoa huduma bora za kisheria