December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rajab Mwenyekiti Mpya CCM Tanga

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Wajumbe wa Mkutano mkuu wa chama cha mapinduzi CCM Mkoa Tanga wamemchagua Rajab Abdulrahman kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa huku akiahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni 14 kwajili ya kulipa posho za makatibu kata na matawi 245 wa Mkoa mzima wa Tanga fedha itakayosaidia kulipa posho za miezi 6 wanayolipwa viongozi hao.

Rajab Abdulrahman ametoa ahadi mara baada ya kuchaguliwa kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa ccm Mkoa Tanga kwa kupata kura 1340 kati ya kura halali 1384 huku kura 6 zikiharibika huku akiburuza wapinzani wake Mathias Mkingwa aliyepata kura 29, na Derick William akipata kura 9.

Mwenyekiti Rajab amesema kuwa makatibu kata hao wanalipwa shilingi elfu 10 kila mwezi kwajili ya shughuli za kukiendesha chama katika ngazi ya matawi na kata na hivyo amewaomba makatibu kata hao na tawi waendelee kuvumilia na kufanya shughuli za chama cha mapinduzi wakati wakitafuta namna bora ya kuendeleza uchumi wa chama hicho.

“Mara nyingine fedha hii imekuwa ikichelewa hali ambayo kwa namna moja au nyingine inapunguza kasi ya uendeshaji wa chama hivyo nimeiona changamoto hii na ninaahidi kuanza nayo pamoja na kuimarisha vyanzo vya mapato ya ndani ya chama, “alisistiza Rajab.

Nataka niseme hivi wakati tuko kwenye subira hiyo katibu wa CCM nikuombe nimepiga hesabu tuna kata 245 mkoa mzima kila kata ukiipa elfu kumi maana yake umetoa milioni mbili kwa mwezi naomba nikukabidhi pesa ya miezi 6 milioni shilingi 14 ili kuanzia mwezi huu tuweze kuipunguza changamoto hii na makatibu kata wapate posho zao kwa wakati.

“Posho anayopewa katibu kata Shilingi elfu 10 kwaajili ya shuguli za chama cha mapinduzi posho hii ni ndogo kwa sababu ya uchumi wa chama chetu ni ndogo lakini pamoja na udogo wake pesa hiyo haifiki kwa wakati, tuna dhamira tuna kila sababu ya kuungana kwa pamoja kuiboresha miradi ya chama cha mapinduzi”
.

Awali akitangaza matokeo hayo msimamizi Mkuu wa uchaguzi huo ambaye pia ni mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela alisema kuwa kati ya wagombea watatu waliokuwa wakiwania kiti hicho Rajabu Abdulrahman amepata kura halali 1384 Wengine walioshinda katika uchaguzi huo ni mjumbe wa halmashauri kuu ya Taifa Mohammed Salimu Ratco akitetea nafasi yake kwa mara ya pili baada ya kushinda kwa kura 774 kati ya 1385 zilizopigwa akiwagaragaza wapinzani wake chini Hassan Bomboko aliyepata kura 563 na Omari Sempon akishika nafasi ya tatu kwa kura 45 pekee.

Hata hivyo mkutano mkuu wa chama hicho umewachagua wajumbe wa Halmashauri kuu ya mkoa wawili kutoka wilaya 8 za mkoa wa Tanga ambapo kila wilaya wamechaguliwa wajumbe wawili miongoni mwao wakiwa ni Habiba Namalecha diwani wa viti maalumu wa jiji la Tanga pamoja na Nassoro Makau aliyekuwa mwenyekiti wa jumuia ya wazazi wilaya.