December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia: tunaenda kufanyiakazi ripoti ya CAG, TAKUKURU

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DODOMA

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema wanaenda kukaa na kuzifanyia kazi kisawasawa dosari zilizojitokeza kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Ripoti ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Rais Samia ametoa ahadi hiyo leo Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma mara baada ya kupokea ripoti hizo mbili kutoka kwa CAG na ile ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.

“Dosari zilizotolewa tutaenda kukaa na kuzifanyia kazi kisawasawa na mwakani pengine hizo hazitajirudia tutakuwa tumesogea,” amesema Rais Samia.

Amewapongeza kwa kazi hiyo, kwani inaimarisha utendaji kwa Serikali, lakini pia kwa mashirika ya umma na kuwasaidia kupunguza hasara kama walivyosikia mifano ambayo CAG amesema.

“Kama tulivyosikia mashirika mbalimbali pamoja na kwamba yanafanya hasara, lakini yanakwenda mbele, hasara ya mwaka jana, sio hasara ya mwaka huu, hasara ya mwaka juzi, siyo hasara ya mwaka uliofuata, kwa hiyo wanakwenda mbele na tutafika pahali watakuwa hawako kwenye hasara, hawako kwenye faida,  watafika mahali watakuwa kwenye faida,” amesema Rais Samia.

Aidha, amesema wamesikia ongezeko la hati safi, na hiyo ni kwa sababu CAG anatoa ripoti yake na watu wakipata wanaenda kurekebisha na matokeo yake tuna asilimia 99 ya hati safi na moja ndiyo hati chafu.

“Kwa hiyo tunasonga mbele, ripoti hizi zinatusaidia sana. Lakini pia ripoti hizi zinatusaidia kwenye kuongeza ukusanyaji mapato kutokana na vipengele mbalimbali anavyovionesha CAG, lakini pia TAKUKURU,” amesema Rais Samia.

Amesema wakienda huko wanasaidia kuziba mianya ile ya fedha zinakopotelea, rushwa na mengineyo, mapato yanarudi Serikalini, lakini zinasaidia kuimarisha nidhamu ndani ya Serikali na utendaji kazi wa watumishi.

Amepongeza TAKUKURU kwa ubunifu mpya wa uibuaji wa kero kwa kushirikiana na wananchi.

“Wanakwenda kule chini wanashirikiana na wananchi, wanasema wanachukua kero wanazichukua taasisi husika wanazifanyia kazi na zinawasaidia kupunguza kero kwa wananchi na kufanya Serikali iwajibike ipasavyo,” amesema.

Lakini pia alimpongeza CAG kwa uibuaji wa mambo kadhaa na kupendekeza hatua za kuchukua, ingawa amewahimiza kuwa utekelezaji uende kwa haraka.

Amesema yote hayo yanawasaidia kutekeleza maelekeze ya  TAKUKURU na CAG.

Amesema kwenye ripiti hizo changamoto na mafanikio yameainishwa vizuri, kazi kubwa ni kuimarisha uwajibikaji, lakini pia na uwazi na ndicho wanachikifanya.