July 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia, Nyusi wakubaliana kuzidi kuimarisha ushirikiano

*Ni katika nyanja za kibiashara, kuazisha Kituo cha Forodha, wataja maeneo ya kutafari upya, washuhudia kusainiwa hati za makubaliano

Na Penina Malundo, Timesmajiraonline

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Msumbiji zimekubaliana kuongeza uhusiano wa kibiashara hasa kwa kuanzisha kituo kimoja cha forodha ambacho kitahamasisha ufanyikaji wa biashara baina ya nchi hizo mbili.

Rais Samia amesema husiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili bado upo , hivyo wataongeza mahusiano hayo pamoja na uwekezaji.

Aliyasema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumkaribisha Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi ambaye yupo nchini kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu.

Rais Samia alisema mwaka juzi (2022) mahusiano ya kibiashara baina ya nchi hizo mbili yalikuwa Dola za Marekani Milioni 57.8, lakini mwaka jana yameshuka hadi kufikia Dola z
Milioni 20.1 ,hivyo wamekubaliana kuangalia sababu zilizosababisha jambo hilo.

“Hii imetushtua wote hivyo tumesema tupaangalie vizuri, tumekubaliana kuangalia ni sababu gani zilisababisha jambo hilo, je usalama ulidhorota biashara zikawa hazipiti katika baadhi ya mipaka, au inawezekana baadhi ya miamala ilifanyika na haipatikani kwa urahisi huko mipakani, hivyo tukakosa takwimu,” alisema Rais Samia

Alisema wapo wawekezaji wawili tu kutoka Msumbiji waliowekeza hapa nchini huku Watanzania 16 ndio waliowekeza nchini Msumbiji na kubainisha kuwa namba hiyo wameiyona ni ndogo hivyo inapaswa kuongezwa.

Aidha, alisema wamekubaliana pia kuongeza ushirikiano wa kuziunganisha nchi hizo mbili na zingine za Afrika katika masuala ya usafiri, usafieishaji na nguvu ya umeme.

“Pia tumekubaliana kushirikiana katika Uchumi wa bluu kama mnavyojua Msumbiji ina Trilioni 100 za ges,i huku Tanzania tuna Trilioni 57 hivyo tumekubaliana kufanya kazi kwa pamoja ili kuona tunawezaje kuiendeleza sekta hii kwa manufaa ya nchi zetu hizi mbili,” alisema

Rais Samia alimshukuru Rais Nyusi kwa kukubali mwaliko wake wa kuja kutembelea Tanzania na kufungua maonesho ya sabasaba.

Kwa Upande wake ,Rais Nyusi alisema wamekutana na Rais Samia na kufanya mazungumzo mbalimbali ikiwemo s kupitia upya suala la ushirikiano wao.

Alisema wanahitaji kufanya juhudi zaidi kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.’

‘Rais Samia ametualika katika maadhimisho ya ufunguzi wa maonesho ya Sabasaba kesho huu ni muelekeo huo huo wa uimarishaji wa ushirikiano wetu kati ya nchi zetu hizi mbili,”alisema

Alisema mazungumzo mengine yalilenga suala la uchumi, kutokana na nchi hizo mbili kupakana wanahitaji kufanya kazi kwa pamoja na wakati mwingine kuwa na mkutano wa pamoja na kuzungumzia namna gani wanaweza kukuza uchumi wa nchi hizo.

Rais Nyusi alisema katika mazungumzo yao pia walizungumzia ziara ya Rais wa Guine Bissau Umaro Embalo ambaye alianza ziara yake nchini Msumbiji na baadae kuja Tanzania na kuzungumza mambo mbalimbali.

Alisema kupitia ziara hiyo ya Rais Embalo kwa nchi ya Msumbiji na Tanzania waliona wanatakiwa kufanya kazi kwa pamoja na kuona namna gani wanaweza kufanya kazi ya kuzalisha zaidi zao la Korosho .

Alisema wanachokiona bidhaa hizo zikichukuliwa na wenzao na wao kutonufaika ipasavyo.

”Hivyo ni vema kuwepo kwa utafiti unaoweza kutafuta namna bora ya zao hili kuleta manufaa kwa nchi zetu,”alisema

”Hivyo ni muhimu kuwa na umoja wa nchi zinazozalisha korosho ambapo zao hili linaweza kuja kuwa na tija hapo baadae,”alisema

Mbali na hayo pia alisema walizungumzia umuhimu wa miundombinu kama uwepo wa daraja la Umoja lililojengwa muda mrefu na kuunganishwa nchi hizo mbili.

”Tunatakiwa kufikilia ni namna gani tunaweza kujenga barabara zaidi zinazotuunganisha,ila sisi kule Msumbiji tumeanza mradi wa Ujenzi kutoka Mueda ambayo itaunganisha nchi yote ya Msumbiji hadi kuja Maputo,”alisema

Alisema ujenzi huo wa miundombinu hiyo ya barabara inalengo la kutimiza adhima ya viongozi wao waasisi ambao walikusudia kuiona Afrika iliyoungana na inayounganishwa.

Alisema kupitia ujenzi huo wa barabara wanaweza kuwa na muunganiko wa Bara la Afrika kutoka Cairo hadi Afrika Kusini, ambapo hata wao wanaweza ingia katika muunganiko huo.

Akitolea mfano wa muunganiko wa barabara hizo kuwa mtu anaweza akasafiri kutoka Tanzania hadi Mueda na kufika katika maeneo mengine Msumbiji.

”Uwepo wa miundombinu hii itawezesha miundombinu mingi ikiwemo miradi ya kiuchumi kama migahama na shughuli nyingine za kiuchumi tunahitaji miundombinu kufanikisha yote hayo,”alisema.

Aidha alisema walizungumzia ushirikiano katika eneo la nishati ambayo inaweza kupitia hata umeme wa Jua(Solar)hivi karibu watakuwa na mradi ambao unaleta ushirikiano wa nchi hizo na kufanya nchi hizo kuwa imara zaidi.