Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOline, Hanang
RAIS Samia Suluhu Hassan, ameelekeza nguvu zote za Serikali zielekezwe wilayani Hanang mkoani Manyara kwa ajili ya uokozi na kuzuia maafa zaidi yaliyosababishwa na mafuriko kutokana na mvua iliyoanza kunyesha usiku wa kuamkia leo.
Rais Samea ametoa maelekezo hayo leo akiwa nje ya nchi anakohudhuria mkutano wa mazingira. Hadi saa saba mchana watu 20 walikuwa wamethibitika kupoteza maisha na mwengine zaidi ya 70 kujeruhiwa.
Mafuriko hayo yametokea katika eneo la Katesh na Gendabi wilayani Hanang mkoani Manyara, ambapo mvua hiyo ilisababisha kuporomoka kwa sehemu ya Mlima Hanang,
Rais Samia amesema kwa masikitiko makubwa wamepokea taarifa za kutokea mvua kubwa katika mkoa wa Manyara na kuleta madhara katika Kijiji cha Katesh.
Ameema wao ambao wanashiriki mkutano wa mazingira, wamesikitishwa sana wametoa pole kwa wahanga wa tukio hilo.
Amesema vyombo vya ulinzi na usalama tayari vimefika huko, Wizara ya afya kwenda kushughulikia majeruhi.
Aidha, ameitaka Wizara ya Madini kwenda kuona katika milima ambayo imeonesha kutetemeka au kuromoka.
“Kwa hiyo nguvu zote zitakuwa huko, nimemtaka Waziri anayeshughulika na maafa aweko huko, kwani ni imani yangu kuwa Serikali ikiwako huko, ni imani yake huduma zinazohitajika zitakuwa zimepatikana,” amesema.
Amewapa pole wananchi wote na kusema yupo njiani kuja kushirikiana nao. Wakati Rais Samia, akitoa maelekezo hayo juhudi kubwa za uokoaji zilikuwa zikiendelea huku waokoaji wakikabiliwa na changamoto mbalimbali.
Aidha, watu wengine wamenusuru uhai wao baada ya kupanda juu ya paa, huku shughuli nyingi. Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja, amesema hadi mchana miili 20 ilipatikana na majeruhi 70 walikuwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tumaini.
Aidha, mafuriko hayo yalibomoa nyumba, kusomba mifugo na kuharibu mali nyingine. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hanang, Rose Kamili, amesema kazi uokoaji bado ni gumu, kwani maeneo mengi hayafikiki.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amethibitishia kutokea kwa vifo na tayari timu ya uokozi imekwishafika eneo la tukio kwa ajili ya kutoa msaada.
Sendiga amesema hadi jana asubuhi vifo vya watu watano vilithibitishwa, wengine 12 kujeruhiwa, ambapo baadhi ya nyumba zilizingirwa na maji.
Amesema alikuwa kwenye ziara wilayani Kiteto, lakini alilazimika kukatisha ziara hiyo kuelekea kwenye tukio. Alisema Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Damas Kayera alikuwa eneo la tukio kwa ajili ya kutoa huduma.
Amesema timu za uokoaji zikiongozwa na Jeshi la Zimamoto na uokoaji zimeshafika eneo la Mji Mdogo wa Katesh wilayani humo kwa ajili ya uokoaji na majeruhi wapo Hospitali ya Wilaya ya Hanang ya Tumaini.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Rose Kamili amesema athari zilizozopo eneo la Gendabi, zinafanana na za volcano iliyotokea miaka iliyopita.
“Maporomoko ni makubwa, mawe, miamba, miti mikubwa na tope yamezoa nyumba nyingi, tumeshindwa kufika kwani hali si shwari, hapaendeki,” alisema Kamili.
“Pia hata maeneo ya Katesh, Gedan’gonyi nyumba nyingine zimefukiwa na tope, miti na mawe,” amesema Kamili.
Mkazi wa eneo la Jorodom wilayani Hanang, Hamis Juma alisema katika eneo lake kuna msiba tayari uliosababishwa na mafuriko kwani mama mmoja amefariki dunia baada ya nyumba kusombwa na maji na watoto wake hawaonekani.
“Watu wamefariki na wengine wamepanda juu ya mapaa ya nyumba na mabasi yanayopita njia ya Arusha kwenda Singida yameshindwa kuendelea na safari,” alisema Hamis.
Mmoja kati ya wasafiri kwenye barabara ya Arusha- Singida, Amina Ally alisema wamesitisha safari kwa muda, kutokana na athari za mvua hiyo ya jana.
Aidha, shule tatu zimetumika kuwapa hifadhi waathirika wa mafuriko hayo, huku wananchi wakitakiwa kuendelea kuchukua tahadhari na kuwasaidia waathirika wa mafuriko.
More Stories
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia