Na Penina Malundo,Timesmajira
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi 12 zitakazozindua Mpango Mahususi wa kitaifa kuhusu nishati,ambapo kupitia mpango huo nchi inatarajia kuongeza kasi ya kuunganisha umeme hadi kufikia asilimia 75 ifikapo mwaka 2030.
Amesema ili kufanikisha adhma hiyo ndani ya muda wa miaka mitano ijayo nchi itahitaji uwekezaji wenye thamani ya dola za Marekani Bilioni 13, ambapo dola bilioni tano zitapatikana kutoka sekta binafsi za hapa nchini.
Rais Samia aliyasema hayo wakati akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika ambao ulianza Januari 27,mwaka huu na kumalizika jana.
Rais Samia amesema kupitia mpango huo mahususi Tanzania imepanga kutekeleza mambo makubwa manne ikiwemo kuongeza uzalishaji wa umeme kutokana na nishati mchanganyiko.
”Hadi sasa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha megawati za umeme 3,431 ambapo asilimia 58 ya hizo zinatokana na vyanzo vya maji, asilimia 35 inatokana na gesi huku asilimia saba inatokana na vyanzo vingine.
”Shabaha ya nchi ni kuongeza megawati 2,463 za nishati ya jua, gesi asilia, upepo, joto ardhi na vyanzo vingine ifikapo mwaka 2030,”amesema.

Aidha alisema kwa upande wa kijografia Tanzania ni kiungo muhimu katika kuunganisha mtandao wa umeme kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika na hivyo kuwezesha biashara ya umeme kutoka Afrika Kusini hadi Misri.
”Tayari tumekwisha unganisha miundombinu ya umeme na nchi za Burudi, Kenya na Rwanda na sasa tunaendelea kuunganisha miundombinu ya umeme na nchi ya Zambia na Uganda.
‘Kuwepo kwa miundombinu hiyo itawezesha biashara ya nishati Kati ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kufanyika,”alisema.
Rais Samia alisema Tanzania inayo nafasi ya kuuza umeme ikizingatiwa kuwa hadi Novemba mwaka 2024, mahitaji ya umeme nchini yalikuwa megawati 1,888 wakati uzalishaji ukiwa megawati 3,431.
Alisema Tanzania inahitaji kufikisha umeme kwenye vitongoji baada ya kufanikiwa kupeleka nishati hiyo katika vijiji vyote vilivyopo nchini.
”Mwelekeo wetu ni kuvifikia vitongoji 64,359 lakini hadi sasa tumeshavifikia vitongoji 32,827 na kazi inaendelea katika vitongoji 20,000 na kupitia mpango huu tunatarajia kuvifikia vitongoji 11,532 vilivyobakia,” alisema Rais Samia.
Alisema mpango huu utasaidia usambazaji wa nishati safi ya kupikia na watu wengi barani Afrika wanakosa nishati safi ya kupikia hali ambayo inaligharimu bara kuhusishwa na kuongezeka kwa umasikini, vitishio vya kiafya, uharibifu wa mazingira,kuongezeka uzalishaji wa kaboni, kupotea kwa baonuai na kukosekana kwa usawa wa kijinsia.
”Nchini Tanzania utegemezi wa kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia ni zaidi ya asilimia 90,hatuwezi kupuuza madhara na gharama kubwa ya kutumia kuni na mkaa hasa kwa afya na ustawi wa wanawake na wasichana.
”Katika kukabiliana na hilo Tanzania tumeweka mkakati wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia unaolenga kupandisha kiwango cha matumizi ya nishati safi ya kupikia toka asilimia 10 ya sasa hadi asilimia 80 ifikapo 2034,”alisema.
Rais Samia alionesha wasiwasi kuhusu hali ya upungufu wa nishati barani Afrika, ambapo takriban watu milioni 600 hawana umeme, na hii inachangia asilimia 83 ya upungufu wa nishati duniani.
Ameweka wazi kuwa wakati sehemu nyingine za dunia kama Asia Mashariki zimefanikiwa kufikia asilimia 96.6 ya upatikanaji wa umeme, Afrika bado iko nyuma, ambapo hadi 2030, watu milioni 545 wataendelea kuwa bila umeme ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa.
“Tutahitaji hatua madhubuti kwa kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya nishati, kuanzia uzalishaji wa umeme hadi kuunganisha umeme katika maeneo ya mbali. Tunahitaji mpango wa pamoja kati ya nchi za Afrika, washirika wetu, na sekta binafsi,” amesema Rais Samia.
Naye Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinumwi Adesina amesema upatikanaji wa umeme ni jambo la muhimu katika bara la Afrika na ukosefu wa nishati hiyo unadhohofisha uchumi wa nchi.
Amesema asilimia kubwa ya Waafrika kwa sasa hawana umeme na ndio maana wameleta ajenda hiyo ya Mission 300 ili kuhakikisha watu wanafikiwa na huduma hiyo ili kukuza uchumi wa nchi za Afrika.
Dkt. Adesina amesema hawataweza kufanikiwa jambo hilo kama hawataweza kufanya kazi pamoja na sekta binafsi na ndio maana wamefika katika mkutano huo kukubaliana ni kwa namna gani watatekeleza jambo hilo la kuwafikishia umeme watu ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kutengeneza ajira.
“Benki ya Dunia (WB) na AfDB tunalenga kutoa dola za Marekani Bilioni 40 kama kianzio cha kuhakiksha tunafanikiwa katika Mission 300,”amesema.
Naye Rais wa Benki ya Dunia (WB), Ajay Banga amesema mikakati yao ni kujielekeza katika kubadili maisha ya Afrika na Mpango wao ni kuhakikisha watu milioni 300 Afrika wanapata umeme ili wawe kichocheo cha upatikanaji wa ajira.
More Stories
Fyandomo:Mama Samia Legal Aid Campaign suluhisho kwa wananchi
Kisa kodi ya pango wafanyabiashara msikiti wa Ijumaa waiangukia Serikali
Kikwete azindua shule ya ghorofa