October 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia mgeni rasmi kumbukizi ya Mkapa 

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya kumbukizi ya Rais wa Serikali ya Awmau ya tatu, Hayati Benjamini Mkapa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu, Benjamin Mkapa Foundation (BMF)Dkt. Ellen Mkondya-Senkoro amesema kumbukizi hiyo yenye jina la Mkapa Legacy Summit inategemewa kufanyika kwa siku tatu kuanzia Julai 29-31 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) ambayo imebeba kaulimbiu isemayo; ‘Kuchagiza uendelevu wa ndani kuelekea upeo mpya’

“Kauli mbiu ya Kumbukizi ya mwaka huu ni ‘Kuchagiza Uendelevu wa Ndani kuelekea kwenye Upeo Mpya’ (Mkapa’s Legacy: Taking local sustainability to new horizons”). Kauli mbiu hii inaangazia maono na kazi mbalimbali za Hayati Benjamin Mkapa katika kuongeza chachu ya maendeleo ya ndani ya nchi, kwa kutumia raslimali, sera na mifumo ya ndani katika kuleta maendeleo.

Maono haya aliyaishi Mkapa, akiamini kuwa Afrika yote ina uwezo wa kujiletea maendeleo yake yenyewe kwa kuzingatia vyanzo na rasilimali zake za ndani, ikichagizwa na mashirikiano na marafiki wa maendeleo wa ndani na nje ya Afrika.” Amesema.

Dkt. Senkoro amesema washiriki takribani 500 wanategemewa kuhudhuria mkutano wa wataalamu wa Afya kuanzia Julai 29-30 huku viongozi 500 wanategemewa kushiriki siku ya kumbukizi ya Hayati Benjamini William Mkapa Julai 31.

Ameongeza kuwa Mkutano huo utawaleta wadau mbalimbali kutoka Serikalini, Wadau wa maendeleo, sekta binafsi, Vyuo Vikuu, wataalamu wa sekta ya afya, pamoja na Mashirika yasiyo ya Kiserikali.

Amesema Lengo kuu ni kubadilishana uzoefu, maarifa, kubaini fursa za masomo na ajira za ndani na nje ya nchi kwa wataalam wa afya, na pia kupendekeza mikakati ya pamoja ya kupunguza changamoto za raslimali watu katika sekta ya afya nchini.

“Wageni wanaotarajiwa kushiriki kilele cha Maadhimisho haya tarehe 31 Julai 2024, ni pamoja na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi,  Familia ya Mkapa, viongozi wa Serikali na Sekta Binafsi, marafiki wa  Mkapa wa ndani na nje ya nchi, Wawakilishi wa Asasi zisizo za Kiserikali, Wadau wa Maendeleo, Viongozi wa Dini, Wataalamu wa Afya wa sekta mbalimbali, wananchi mashuhuri, Waandishi wa Habari n.k.”

Pia amesema Mwaka huu, kumbukizi hii itaanza kwa majadiliano ya kitaifa ya kitaalamu ya siku mbili juu ya masuala ya rasilimali watu katika sekta ya afya, yaliyopewa jina la “National Human Resource for Health (HRH) Conference”.

” Majadiliano haya yatafanyika Julai 29-30, 2024 kuelekea kilele cha Kumbukizi kitakachoadhimishwa Julai 31,2024 ambapo suala la rasilimali watu katika sekta ya afya ndio linalobeba dhima ya mkutano.”

“Kwa sasa Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi zinazohusiana na watumishi wa afya ikiwemo pia upungufu wa takribani asilimia 66 ya watumishi wa afya katika vituo vya kutolea huduma za afya. Kukabiliana na hizi changamoto hatuna budi kuunga mkono jitihada za Serikali tukiwa kama wadau wa sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kutatuamapungufu hayo.”

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi Mkapa Foundation, Rahel Sheiza, amesema sambamba na maadhimisho hayo, Taasisi hiyo itazindua mpango mkakati wao wa nne ambao pia unatoa taswira nzima ya ushirikishwaji wa wadau katika Sekta mtambuka kuboresha huduma zao za Afya na kuchangia katika Mipango mikakati ya maendeleo nchini

Pia amesema kutakua na uwasilishaji wa vielelezo na utafiti kutoka kwa wadau wa Sekta mbalimbali ambazo zinachangia kwenye Sekta ya afya ambapo lengo lake kuu ni kuboresha katika kuhakikisha kwamba Wana tija, ubora na uthabiti wa huduma ambazo wanazitoa za afya.

Kadhalika, Sheiza amesema watapata nafasi ya kukutanisha mabalozi wanaoiwakilisha nchi katika nchi mbalimbali kuja kujadili na kubadilishana mawazo kwenye fursa adhimu za kidiplomasia na kimaendeleo

Naye Mwakilishi Wizara ya Afya, Asnath Mpelo,  alisema kama wizara ambayo inasimamia Sekta ya Afya alikiri kuwepo kwa uhaba wa watumishi katika Sekta ya afya kwa takribani asilimia 65 ukilinganisha na mahitaji hivyo serikali imeendelea kuwa na juhudi mbalimbali kuweza kuziba pengo hilo ikiwemo kushirikiana na wadau katika maeneo mbalimbali wakiwemo Mkapa Foundation ili wananchi waweze kupata huduma bora na stahiki.