Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Dar
RAIS Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), anatarajiwa kuongoza mkutano wa 12 wa Baraza hilo ambao utafanyika Jijini Dar es Salaam kesho kutwa (Jumamosi).
Pamoja na mambo mengine utaangazia masuala ya kodi, mamlaka za udhibiti pamoja mazao yatokanayo na misitu.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dkt Godwill Wanga amesema kauli mbiu ya mkutano huo muhimu unaowakutanisha wajumbe kutoka sekta za umma na binafsi itakuwa; “Ufanisi wa Biashara na Uwekezaji katika Uchumi wa Kati, Kazi Iendele.”
“Huu ni mkutano muhimu sana, kwani mbali ya mambo mengi, wajumbe wa mkutano na hasa wale wanaotoka sekta binafsi watapata fursa ya kipekee kumkaribisha mwenyekiti wa Baraza ambaye ataongoza mkutano wa Baraza kwa mara ya kwanza,” amesema Dkt. Wanga.
Dkt Wanga amesema mkutano wa Jumamosi utafuatiwa na mkutano mwingine Jumapili utakaongonzwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambao pamoja na mambo mengine utapitia mapendekezo ya mkutano wa Rais na pia kutathimini siku 100 ya mafanikio na utendaji wa Rais Samia tangu aapishwe kuwa rais.
“Watendaji wakuu Serikalini wakiwemo makatibu wakuu,mawaziri na viongozi kutoka sekta binafsi watashiriki kwenye mkutano huu wa kesho ambao maandalizi yake yameshakamilika,” amesema Dkt. Wanga.
“Mkutano huu ni fursa pekee kwa wajumbe kutoka sekta za umma na binafsi ambao kwa ujumla wao wataangalia namna ya kuboresha ushindani wa biashara kitaifa na maendeleo ya kiuchumi,” amesisitiza na kuwaomba wadau mbalimbali kuendeleo kumuunga mkono Rais Samia katika utekelezaji wa majukumu yake.
Akisisitiza zaidi kuhusu mkutano wa baraza, Dkt Wanga amesema Baraza litaendelea kusimamia mazingira mazuri ya ushindani kibiashara ili kuvutia zaidi uwekezaji sambamba na kuimarisha ujenzi wa viwanda hapa nchini.
“Wajumbe wa mkutano wataangalia pia namna ya kupunguza mzigo wa gharama za uendeshaji wa biashara kwa wajasiriamali wadogo na wakati (SMEs) ili kuleta chachu kwa uongozaji wa ajira kwa sekta binafsi ambayo ni muhimili mkubwa wa uchumi,” alisema.
TNBC ni chombo muhimu cha majadiliano kati ya sekta za Umma na Binafsi ambacho hutoa fursa pekee kwa viongozi kutaka pande hizo mbili kuhusu mambo mbalimbali namna ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini pamoja changamoto zake.
Kimuundo Baraza lina wajumbe idadi sawa kutoka sekta za Umma na Binafisi ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano ni mwenyekiti wake na Makamu wa Mwenyekiti wa Baraza anatoka sekta binafsi.
More Stories
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi