December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia azindua tovuti ya nyaraka za Dkt. Salim Ahmed Salim

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekibadilisha jina Chuo cha Diplomasia nchini na kukipa jina la Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim.

“Na kwasababu mcheza kwao hutunzwa, na tumesema alikuwa mwanadiplomasia mahiri, tumekubaliana kukipa Chuo kile cha Diplomasia jina na sasa rasmi kitakuwa kinaitwa Dr. Salim Ahmed Salim Centre for Foreign Relations.”

Aidha, Rais Samia amesema lengo la kukipa jina hilo ni kuonesha mchango uliotolewa na mwanadiplomasia Dkt. Salim ambae alifanya kazi kwa muda mrefu katika nyanja ya kidiplomasia ya kimataifa kwa nidhamu bila kukata tamaa.

Rais Samia amesema hayo leo kwenye hafla ya uzinduzi wa tovuti ya nyaraka za Dkt. Salim Ahmed Salim, iliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.

Rais Samia amemuelezea Dkt. Salim kama kiongozi aliyethamini elimu katika jamii na aliyesaidia watu wengi kufikia maendeleo na ndoto zao kwa kutoa ushauri na mafundisho mbalimbali.

Rais Samia ameeleza kuwa katika uongozi wake, Dkt. Salim alitoa mchango mkubwa katika uhamasishaji wa masuala ya uzalendo, muungano na umoja ambao yalichangia katika kudumisha amani na umoja wa taifa.

Rais Samia ametoa wito kwa viongozi wa umma kuiga mfano wa Dkt. Salim kwa kutunza kumbukumbu za maisha yao kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadae ili zisaidie kukuza na kuimarisha uelewa wa juhudi za kila kiongozi, historia ya nchi na bara la Afrika.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akipata maelezo juu ya historia ya Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim kwenye bango maalum kabla ya kuzindua Tovuti ya Hifadhi ya Nyaraka za Kumbukumbu za Kidigitali za Kiongozi huyo kutoka kwa mtoto wake wa kiume, Ahmed Salim kwenye hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na wanafamilia wa Dkt. Salim Ahmed Salim mara baada ya kuzindua Tovuti ya Hifadhi ya Nyaraka za Kumbukumbu za Kidigitali za Kiongozi huyo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa hafla ya uzinduzi wa Tovuti ya Hifadhi ya Nyaraka za Kumbukumbu za Kidigitali za Dkt. Salim Ahmed Salim iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba, 2023.
Sehemu ya wanafamilia ya Dkt. Salim Ahmed Salim wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa Tovuti ya Hifadhi ya Nyaraka za Kumbukumbu za Kidigitali za kiongozi huyo iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan pamoja na Ahmed Salim mtoto wa kiume wa Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim, wakifuatilia kwa makini video fupi ya kumbukumbu mbalimbali (hazionekani pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi wa Tovuti ya Hifadhi ya Nyaraka za Kumbukumbu za Kidigitali za Dkt. Salim Ahmed Salim iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba, 2023.
Mwezeshaji wa mjadala juu ya kumbukumbu ya Dkt. Salim Ahmed Salim, Profesa Saida Yahya Othman akiongoza mjadala uliochangiwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Joseph Warioba, Balozi Christopher Liundi na Balozi Amina Salum Ali wakati wa hafla ya uzinduzi wa Tovuti ya Hifadhi ya Nyaraka za Kumbukumbu za Kidigitali za Dkt. Salim Ahmed Salim ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa Tovuti ya Hifadhi ya Nyaraka za Kumbukumbu za Kidigitali za Dkt. Salim Ahmed Salim kwenye hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba, 2023.