Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Zanzibar
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amekabidhiwa na kuizindua Skuli ya Maandalizi iliyopewa jina lake, iliyopo Kijiji cha Tasani, Makunduchi, Zanzibar, iliyojengwa na Benki ya NMB kwa gharama ya Sh. Bilioni 800.
Jiwe la msingi la ujenzi wa Skuli ya Dk. Samia Suluhu Hassani liliwekwa Agosti 29, 2023 na Rais Samia mwenyewe, wakati wa Tamasha la Kizimkazi la mwaka jana, ambako NMB ilitarajia ingegharimu kiasi cha Sh. Mil. 600, lakini kutokana na kuongezeka kwa maeneo ya ujenzi na samani za ndani, skuli hiyo imekamilika ikigharimu Sh. Mil. 800.
Akipokea na kuzindua Skuli hiyo, Rais Samia alikiri kuvutiwa sio tu na ufadhili wa NMB kujenga shule hiyo, bali mchango wa jumla wa taasisi hiyo katika Tamasha la Kizimkazi 2024, ambako imefanya mambo mengi na makubwa ikiwemo uzinduzi wa miradi mbalimbali na kufichua kuwa Serikali yake inautegemea sana uwepo wa benki hiyo kama mdau kinara wa maendeleo.
“Tunaishukuru sana NMB sio tu kwa hili, bali kwa ujumla wake imetoka mchango mkubwa katika Kizimkazi Festival, kama ambavyo Afisa Mtendaji Mkuu alivyobainisha, wamefanya makubwa sana, kote Wilaya ya Kusini kuna miradi yao inayofanana na huu. Nataka niseme Serikali tunategemea sana uwepo wao kwa ajili ya usaidizi wao.
“Licha ya kazi kubwa waliyofanya katika mradi huu na waliyofanya kwenye Tamasha hili kwa ujumla, zaidi niwapongeze kwa kutambuliwa Kimataifa na kupewa tuzo mbalimbali, zikiwemo mlizopewa na Jarida la Euromoney.
“Nimesoma ‘article’ za Euromoney ikiwatambua NMB kuwa ndio Benki Bora Tanzania na pia ndio Benki Inayojali Mazingira, Jamii na Utawala Bora, na hapo katika jamii, Skuli hii ni sehemu ya mfano hai wa uwajibikaji wao kwa jamii. Wanafanya hivi kwa sababu jamii ndio iliyowafikisha walipo, wanapata faida kubwa na kutenga fungu la kurejesha kwa jamii hiyo.
“NMB wangeweza kukaa na faida yao yote, lakini kwa kujali kwao, wamechagua kurejesha kwa jamii sio tu ya Wazanzibar, bali Watanzania wote. Natamani taasisi zingine zingefuata nyayo za NMB katika kuitumikia jamii kupitia faida wanazopata,” alisema Rais Samia.
Awali, Rais Samia alisema Skuli hiyo ni zao la kaulimbiu ya Kizimkazi Festival 2023 ya: ‘Tuwalinde Watoto Wetu kwa Maslahi ya Taifa’ na kwamba ujenzi wa shule bora na ya kisasa uliofanywa na NMB unatekeleza kwa vitendo Sera ya Afya ya Uzazi inayozingatia makuzi sahihi na ustawi watoto katika siku 1,000 za awali tangu kuzaliwa hadi wanapoanza elimu ya awali.
Akikabidhi Skuli hiyo kwa Rais Samia, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema wanayo furaha kubwa kukamilisha kwa wakati ujenzi wake na kuipa jina la Rais, ingawa umekuwa wa gharama kubwa kuliko ilivypangwa awali, kuwa gharama za Sh. Mil. 800 zimejumuisha ongezeko la ujenzi wa sehemu ya chakula, ununuzi wa samani kwa ajili ya walimu na wanafunzi, uwekaji wa viyoyozi katika ofisi ya walimu, sehemu ya paredi na sehemu ya kuchezea watoto zikiwemo bembea.
“Ongezeko hilo la thamani limetokana na ujenzi huo wa ziada ambao haukuwa katika mpango wa awali uliojumuisha madrasa matano, ofisi ya Mwalimu mkuu, ofisi ya walimu, stoo, na miundombinu ya majisafi na majitaka, lakini kwa kutambua umuhimu wa vitu vilivyoongezwa, tukaona ni vyema kuongeza gharama hizo, ili kuifanya shule hiii iwe na viwango bora vinavyohitajika kwa ajili ya watoto wetu.
“Kwetu sisi NMB, Skuli hii ni alama ya matumaini na ndoto mpya kwa watoto wa eneo hili, ambao watajengewa msingi imara wa elimu, tukiamini kuwa kupitia elimu, tunaweza kuleta mabadiliko makubwa katika jamii yetu na kuandaa viongozi wa kesho wenye uadilifu, maarifa, uzalendo,” alisema Bi. Zaipuna.
Aliongeza ya kwamba mradi huo unaotokana na Sera ya NMB ya Uwajibikaji kwa Jamii, ni muendelezo wa mchango wao mkubwa walioutoa katika Sekta za Elimu, Afya, Usaidizi wa Changamoto za Majanga na Vifaa Saidizi vya Walemavu, huku akichanganua kwa kutaja mambo iliyofanya katika nyanja zote.
“Benki yetu inatenga asimilia moja ya faida yake baada ya kodi ili kusaidia sekta hizo za kimkakati, ambapo tangu Januari hadi Juni mwaka huu, tumeboresha mazingira ya shule mbalimbali za Serikali bara na visiwani Zanzibar, kwa kutoa madawati, viti na meza za walimu, kuezeka madarasa.
“Aidha, tumetoa zaidi ya madawati 6,420 kwa shule 103 na kuwezesha zaidi ya wanafunzi 19,000 kujifunza wakiwa wameketi kwenye madawati, lakini pia tumetoa pia meza 64 na viti 88 kwa ajili ya waalimu ili kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu,” alifafanua Bi. Zaipuna.
Aliongeza ya kwamba benki yake imezisaidia Skuli 9 vitanda zaidi ya 360 vya kulalia wanafunzi 720, hasa kwa watoto wa kike, huku kupitia NMB Foundation, ambayo ni asasi isiyo ya kibiashara ya benki hiyo, inasomesha vijana wa Kitanzania 130 katika vyuo vikuu mbaimbali nchini.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini