September 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia azidi kutekeleza miradi aliyoanzisha Magufuli

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Updates

RAIS Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya Kaengesa – Chitete (km 6.4) sehemu ya Kaengesa – Seminari (km 3.4) kwa kiwango cha lami Wilayani Sumbawanga.

Dkt. Samia ameweka jiwe la msingi jana Mkoani Rukwa na kukagua hatua zilizofikiwa za ujenzi wa barabara ya Kaengesa – Seminari ambayo ni moja ya ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, ya mwaka 2019 Mkoani humo.

“Tunaposema kazi iendelee ni ujenzi wa barabara hii, Barabara hii ilitolewa ahadi na Serikali ya Awamu ya Tano na sasa awamu ya Sita tunaenda kukamilisha ujenzi wa barabara hii”, alisema Dkt. Samia.

Dkt. Samia aliwaahidi wananchi wa Wilaya ya Sumbawanga kuwa Serikali itakamilisha ujenzi wa Barabara ya Kaengesa – Seminari kwa kiwango cha lami ifikapo Septemba, 2024.

Aidha, Dkt. Samia alitembelea Shule ya Seminari ya Kaengesa na kumuelekeza Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa kutekeleza ombi la Shule hiyo la kuunganisha barabara za lami zinazozunguka shule hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa alisema katika Sekta ya Ujenzi Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kukamilisha miradi yote iliyoasisiwa na Hayati Magufuli.

Alisema barabara hiyo aliyoweka jiwe la msingi ipo katika mtandao wa TARURA lakini ilielekezwa TANROADS kwa kushirikiana na TARURA kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ya Kaengesa – Chitete (km 6.4) na tayari TANROADS wameanza ujenzi wa barabara hiyo kuanzia Kaengesa hadi kufika Seminari (km 3.4) huku upande wa TARURA wakiwa wanakamilisha usanifu wa Kilometa 3.

Awali akitoa taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta ameeleza kuwa barabara ya Kaengesa – Seminari inajengwa na Mkandarasi mzawa M/s Sumry Enterprises kutoka Sumbawanga kwa gharama ya Shilingi Bilioni 6.2 kwa awamu mbili za ujenzi na unasimamiwa kitengo cha TECU Mkoa wa Rukwa.