Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha Tsh. Bil. 9 kwa ajili ya mafunzo ya wataalamu wa fani za ubingwa na ubingwa itayosaidia kukabiliana na changamoto ya upungufu wa fani hizo katika maeneo ya utoaji huduma za afya kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel Jijini Dar es Salaam wakati akiongea na Waandishi wa habari kuhusu mpango wa kila mwaka wa ufadhili wa masomo kwa Wataalamu wa afya katika kada mbalimbali ujulikanao kama “Samia Suluhu Super Specialists Programu”
Amesema, kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ya Rais Samia ilitoa kiasi cha shilingi Bil. 8 katika mpango huo na sasa imetoa Tsh. Bil 9, ni ongezeko la Tsh. Bil. 1.
Dkt. Godwin Mollel amesema, mageuzi makubwa yanazidi kufanyika ndani ya Sekta ya afya lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu ikiwemo yale ya kibingwa na kibingwa bobezi hapa hapa nchini.
“Kwenye eneo la ujenzi, tunaushuhudia uboreshaji wa miundombini, ajira za wataalam, ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, …, unaenda sambamba na kuendeleza taaluma za Wataalam wa Afya nchini ili waweze kutoa huduma bora za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi nchini.” Amesema.
“Wizara ya Afya ilijiwekea lengo la miaka mitano (2020-2025) la kusomesha wataalamu bingwa na bobezi wasiopungua 300 kwa kila mwaka wa fedha. Kupitia mpango huu wa ufadhili wa kuongeza wataalam bingwa na bozezi Tanzania (Samia Health Super Specialisation Program In Tanzania). Ameongeza Dkt. Mollel.
Aidha, Dkt. Mollel amesema Fedha hizi zitatumika kugharamia mafunzo kwa wataalamu bingwa na bobezi 848 wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi, huku akisisitiza Serikali ya Dkt. Samia inatarajia kufadhili Wataalamu wapya wasiopungua 300 kwa utaratibu wa kawaida pamoja na wataalamu wengine wasiopungua 100 kwa utaratibu wa seti (Mfano seti ya; Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura, Muuguzi Bingwa, Dakatri Bingwa wa ganzi na usingizi).
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, maombi yote yawasilishwe kwa njia ya kielektroniki kupitia tovuti na kusisitiza maombi yatakayofanyiwa kazi ni yale yaliyowasilishwa kwa njia ya mfumo tuu, hivyo waombaji wanakumbushwa kufuata utaratibu uliowekwa.
Pia, amebainisha “Ufadhili huu ni kwa ajili ya kulipiwa ada ya mafunzo, posho ya kujikimu na nauli kwa wanafunzi watakaopata ufadhili nje ya nchi.
More Stories
Wenje:Tuwanadi wagombea bila kuchafuana
Mtoto darasa la tatu adaiwa kujinyonga kwa kukosa nguo ya sikukuu
Jeshi la Polisi Katavi laanika mafanikio 2024