May 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia atoa bil.10 ukarabati barabara za ndani Ilala

Na Heri Shaaban,Timesmajiraonline,Ilala

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, ametoa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya miundombinu ya Barabara za ndani  Wilaya ya Ilala.

Mpogolo amesema hayo wakati wa kukagua utekelezaji wa Ilani kwa kukagua miundombinu ya Barabara za wilaya hiyo.

“Wananchi wilayani ilala, Mkoani Dar es salaam, wanaendelea kunufaika na matunda ya Serikali ya awamu ya sita, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 10 za fedha za ndani kujenga  miundombinu ya barabara na madaraja”alisema Mpogolo.

Mpogolo alisema maeneo yanayojengwa miradi hiyo ambayo ni madaraja na barabara katika kiwango cha lami barabara zilizokuwa kero.

Alizitaja barabara hizo zinazonufaika na fedha za ndani ni katika kata ya Liwiti barabara ya Tabata Magengeni, na daraja la Kavesu na daraja la Mzava.

Aidha alisema Kata ya Vungunguti ni barabara ya Faru Mnyamani, Kidarajani, tatanic moja na mbili, huku kata ya Pugu fedha hizo zinanufaisha wananchi kwa ujenzi wa barabara ya Kigogo sokoni na Pugu Kanisani.

Amebainisha kuwa kwa wananchi wa kata ya Kivule fedha hizo za ndani zinajenga daraja la Msumi, bombambili na kata ya Kitunda ujenzi wa miundombinu unafanyika katika barabara ya Mwanagati hadi Kitunda.

Mkuu huyo wa wilaya ya Ilala  Edward Mpogolo, ameongeza kuwa  kwa upande wa jimbo la Ilala, fedha hizo zilizoidhinishwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan zimeelekezwa katika ujenzi wa barabara ya Nyamwezi na Congo kwa kiwango cha lami.

Alisema  kata ya Ilala, ujenzi wa  barabara ya Moshi kwa kiwango cha lami huku kata ya Buyuni  na Chanika wananchi wananufaika na barabara ya Italiani  miti mirefu na masai wawili kwa kiwango cha lami.

Kata nyingine amezitaja ni Kipawa na Buguruni ambazo ujenzi wa barabara katika kiwango cha lami unafanyika eneo la Airport hadi karakata na barabara ya Sukita.

Mpogolo,amesema ili fedha hizo zinazotolewa zionyeshe jita kwa wananchi katika miundombinu ni vema wakawa na matumizi mazuri na kulinda miundombinu.

Huku akitoa wito kwa TARURA wilayani ilala  kuhakikisha wakandarasi wote waliopewa tenda za ujenzi  wanakabidhi miradi inayoendana na thamani ya fedha.

Ameongeza kuwa kupatikana kwa fedha hizo za ndani ni matunda ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia na usimamizi mzuri wa halmashauri ya jiji la Dar es salaam na kuwapongeza wabunge na madiwani wote kuhakikisha maendeleo yanaonekana kwa wananchi.