December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia atembelea Banda la Benki ya Equity, MIF

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametembelea banda la benki ya Equity kwa kushilikiana  na Taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF) wakati wa tamasha za Kizimkazi Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa Habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Isabela Maganga amesema Kizimkazi na Mkoa wa kusini Unguja kwa ujumla ni sehemu ya utekelezaji wao katika kubadilisha maisha ya wananchi kiuchumi na kijamii kwa kuwawezesha vijana ,wanawake, na wajasiliamali wadogo na wakubwa kwa kushilikiana na Taasisi ya MIF. 

Aidha Maganga amesema Ushirikiano wa benki ya Equity na Taasisi ya MIF umelenga kuleta maendeleo Zanzibar kwa watoto wa kike na vijana kwa ujumla.

Amesema Wana lengo la kuwaongezea vijana ujuzi kupitia VETA ikiwa ni kusaidia katika suala zima la nishati na mazingira kwa kuhakikisha kaya zinapata nishati safi za kupikia ili kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuwaepusha na magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya nishati chafu kama kuni na mkaa.

“tutahakikisha vijana wanashiriki kwenye upandaji miti na kulinda vyanzo vya maji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.”

Aidha amesema lengo pia ni kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo wakike haswa ya kifedha na jinsi ya kuendesha biashara zao ili ziweze kukua na kutengeneza faida itakayosaidia kuendesha maisha yao.

Pamoja na hayo, Maganga amesema wataingia makubaliano ya dhamana wezeshi kusaidia kupunguza hatari ya mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati. 

“Wengi wamekuwa wakishindwa kulipa mikopo yao sio kwa sababu biashara mbaya bali ni kukosa elimu ya kifedha.”

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Isabela Maganga wakati alipotembelea Banda la Benki hiyo hapo juzi Zanzibar katika kilele cha Tamasha la kizimkaz.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Isabela Maganga akielezea juu ya mikakati ya benki yetu na ushirikiano na Taasisi ya MIF kwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan apo jana Zanzibar.