February 26, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia ataka watumishi kumaliza adha ya maji kwa wananchi

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Handeni

RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan amewataka watumishi wa Wizara ya Maji kufanya kazi hiyo kwa moyo huku wakikumbuka ndugu zao waliopo vijijini kuwa bado wana shida ya maji.

Dkt.Samia ameyasema hayo leo Februari 25, 2025 kwenye hafla ya uwekaji Jiwe la Msingi Mradi wa Maji wa Miji 28 Mkoa wa Tanga kwenye miji ya Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani kwa hafla hiyo kufanyika mjini Handeni.

Dkt.Samia amesema ni kweli mishahara wanayolipwa wafanyakazi ni midogo, lakini wanatakiwa kufanya kazi kwa moyo ili kuweza kuwasaidia wananchi kuweza kupata maji safi na salama.

Amesema, Wizara ya Maji ilikuwa inaitwa wizara ya lawama, lakini tangu mwaka 2022, kuna mabadiliko makubwa ya kiutendaji, kiuwajibikaji na kimuundo, hivyo kuleta matumaini kwa wananchi, na kutoka kuwa wizara ya lawama na kuwa wizara ya sifa.

“Ulipozungumza (Waziri wa Maji, Jumaa Aweso), sifa zote ulinipa mimi. Lakini mimi nafanya kazi kwenye makaratasi na kutafuta fedha, kazi ya kujenga miundombinu yote ya maji inafanywa na wizara kupitia mainjinia na wataalamu hawa waliokuwepo. Kwa hiyo ile sifa yote ya maji iliyokuwepo kwenye maji, tulivyogeuza Sekta ya Maji, ni sifa yenu, nami nawashukuru sana, sana, sana.

“Naijua Wizara ya Maji ilivyokuwa. Wizara hii ilikuwa inaitwa wizara ya lawama, lakini sasa inaitwa wizara ya sifa, niombe sana muendelee na sifa hiyo. Lakini ndugu zangu hapa mnafanya kazi tunawalipa kidogo… najua mshahara ni mdogo, hautoshi, lakini  wote tumetoka vijijini, tufikirieni hali ilivyokuwa ya mama zetu na dada zetu ilivyokuwa kule tulikokuwa na leo tunavyowasogezea maji karibu kuyatoa tulikoyatoa, tunawapunguzia mzigo wa kiasi gani”amesema Dkt. Samia.

Dkt.Samia amesema kwa kuweza kupeleka maji hayo vijijini wamesaidia vitu vingi ikiwemo kuwasaidia watu kufanya ibada, kwani bila maji itawawia vigumu. Lakini pia maji hayo yanasaidia kuondoa magonjwa ya kuhara na milipuko.

Naye Waziri Aweso amesema Rais Dkt.Samia tangu ameingia madarakani, na baadae kuhutubia Bunge Aprili 22, 2021, alijipambanua kuwa anataka kumtua mwanamke ndoo kichwani, huku akimpa maagizo mazito katikati ya hotuba yake. Hivyo, kama Waziri wa Maji aliyepewa dhamana ya kuwapa wananchi maji, alihakikisha wanapambana kuona wanaondoa shida ya maji.

“Ulipoingia madarakani moja ya jambo kubwa ulilolielekeza katika Bunge tarehe 22/4/2021 ulisema kwamba wewe ni mama, na wanaoteseka na adha ya maji ni akina mama,  hutaki kusikia, hutaki kuona wamama wa vijijini wakiteseka na adha ya maji, na ukanieleza Waziri wa Maji, ukinizingua tutazinguana. Nini maana yake, tunataka kumtua mwanamama ndoo kichwani”amesema Aweso.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amesema Mradi wa Maji Miji 28 kwa Mkoa wa Tanga utahudumia wananchi wa miji ya Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani.

Mhandisi Waziri alisema mradi huo umetokana na mradi uliokuwepo awali wa Handeni Trunk Main (HTM) uliojengwa kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GTZ) na sasa GIZ mwaka 1974, na ulitakiwa ufanyiwe matengenezo makubwa ya miundombinu baada ya miaka 20 yaani mwaka 1994, lakini hakuna matengenezo makubwa yaliyofanyika kwa miaka 48.

Amesema mradi wa awali na wa sasa ambao  chanzo chake ni Mto Pangani, na kidakio (Intake) kikiwa kimejengwa Kijiji cha Mswaha- Darajani wilayani Korogwe, ulikuwa unazalisha maji lita milioni tano kwa siku na kuhudumia wananchi 180,000, lakini mradi wa sasa unakwenda kuzalisha lita milioni 52 kwa siku na kuweza kuhudumia wananchi 860.

Mhandisi Waziri alisema ukiacha miji itakayohudumiwa na maji hayo, vijiji 180 vitavyozunguka bomba hilo pia vitanufaika na maji hayo.