March 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia ataka watakao kwamisha huduma za ardhi kuchukuliwa hatua

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan, amemuagiza Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, kuhakikisha anasimamia kwa umakini utendaji wa sekta hiyo na kuwachukulia hatua watendaji wanaokwamisha huduma za ardhi na kusababisha malalamiko kwa wananchi.

Dkt.Samia ametoa maelekezo hayo jijini hapa leo Machi 17,2025 wakati wa uzinduzi wa Sera ya Ardhi ya Mwaka 1995, toleo la Mwaka 2023,ambapo amesema wafanyakazi waliopo katika sekta ya ardhi hawazungumzwi vizuri huku wakihusishwa na rushwa

Amesema miongoni mwa kero inayotajwa na wananchi ni kuuza kiwanja kimoja mara mbili hivyo teknolojia inayokuja ya utambuzi itasaidia kumaliza hilo na kuwataka kubadilika

Hivyo amesema sera hiyo imeleta maboresho makubwa kwa lengo la kuondoa hizo changamoto zilizokuwepo, hivyo hakuna sababu kwa mtendaji yeyote kuikwamisha.

Pia Rais Samia amesisitiza umuhimu wa Wizara kuendelea kuhakikisha kunakuwepo na nyumba za bei nafuu kwa wananchi sambamba na kufanya maboresho ya makazi kwenye miji na majiji mbalimbali akitolea mfano baadhi ya makazi duni yaliyopo kwenye maeneo ya Jiji la Dar Es salaam ikiwemo Mwananyamala na Kinondoni, akisisitiza umuhimu wa Majiji na Miji kuwa na hadhi na sura ya kuendana na Miji na Majiji.

Pamoja na hayo Rais Samia amesema hakuna sheria inayomkataza mwanamke kumiliki ardhi kwani naye ana haki ya kupata ardhi kama ilivyo kwa mtu yoyote yule kwa kuzingatia taratibu za nchi.

Amesema kuwa mwanamke naye ana haki ya kumiliki ardhi kwa kufuata misingi na taratibu na sheria za nchi kama alivyo mtu mwingine yoyote ilimradi awe ni mtanzania.

Kwa upande wake Waziri wa Ardhi Deogratius Ndejembi amehimiza utekelezaji wa sera hiyo na kusema kuwa ni kati ya sera ambayo itakuwa mlinzi wa matumizi ya ardhi.

Amesema Wizara ya Ardhi na TAMISEMI kwa kushirikiana watahakikisha wanapima ardhi na kubaini nchi ina ukubwa gani na kutambua matumizi bora ya ardhi kwa faida ya vizazi vijavyo.

“Tunatambua kuwa tangu kuwe kwa mipaka ya nchi ardhi haongezeko lakini watu wanaongezeka hivyo Wizara inakila jukumu la kupima kuhakikisha kila kiande cha ardhi kinapimwa na kupangiwa matumizi bora ili kuweka utaratbu mzuri wa kurithisha vizazi vijavyo ” amesema Deogratius.