Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha inaendelea kuzingatia maslahi ya nchi kwenye Mikataba mbalimbali ambayo nchi inakusudia kuingia kwakuwa Kikatiba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiyo yenye dhamana ya Upekuzi na Tathmini ya Mikataba inayongiwa na Serikali na Taasisi zake.
Dkt. Samia ameyasema hayo leo tarehe 03 Februari, 2025, wakati alipokuwa Mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Sheria Nchini 2025 yaliyofanyika katika Viwanja vya Chinangali Jijini, Dodoma.
Aidha, Dkt. Samia amewataka watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kuzingatia Weledi wakati wa kufanya Upekuzi na Tathmini ya Mikataba mbalimbali ambayo Serikali inayokusudia kuingia.
“Katika kuhakikisha masilahi ya nchi yetu yanaendelea kuzingatiwa kwenye Mikataba itakayoingiwa ni lazima Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wawe na uwezo na ubobevu kwenye masharti ya Kimikataba yanayogusa sekta za kiuchumi na uwezo wa kusimamia mikataba hiyo”. Amesema Dkt. Samia
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza S. Johari akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea Kufanya upekuzi na tathmini kwenye Mikataba mbalimbali ambapo kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Desemba 2024 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilikuwa imepekua Mikataba 1,799 na Hati za Makubaliano 352.
“Kati ya mwezi Julai hadi Disemba, 2024 jumla ya Mikataba ya Kitaifa, Kikanda na 10 Kimataifa 1,799 na Hati za Makubaliano (Memoranda of Understanding) 352 zilifanyiwa upekuzi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika hatua nyingine . Johari amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kuwahimiza Mawakili wa Serikali na Wanasheria wote walioko katika utumishi wa umma kujiendeleza na kushiriki mafunzo ya fani mbalimbali.
More Stories
Rais Samia kupokea Tuzo ya ”The Gates Goalkeepers Award”
Walengwa wa TASAF watakiwa kujiandaa ukomo wa ruzuku
Kapinga:Azma ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika wakati wote