January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia aridhishwa na matumizi ya sh.bil 6 katika ujenzi ofisi ya RC Mbeya

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Mbeya

RAIS Samia Suluhu Hassan ameonyesha kuridhishwa na ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa mkoa Mbeya lililojengwa na Wakala wa Majengo TBA lenye thamani ya shilingi Bilioni 6.

Akizungumza wakati akizindua jengo hilo Rais Samia amesema,ameridhishwa na jengo lenyewe lilivyojengwa hata na thamani ya pesa iliyotumika kutokana na muonekano wa jengo hilo.

“Nilipomabiwa utafungua na kuweka jiwe la msingi jengo la Mkuu wa Mkoa Mbeya, nikajua ni jengo jengo tu hivi,nikarushiwa mapicha nikasema mmmmh…kweli, nimefika nimeshuhudia kazi nzuri mliyoifanya ,ni jengo la aina yake, kwa hiyo nimeridhika pesa jinsi ilivyotumika

“Nataka niwaambie kwenye utawala bora hii ndiyo kazi serikali inafanya ,kuboresha maeneo ambayo wananchi wanakwenda kuhudumiwa ili wakiingia wajue kwamba wameingia mahali na wapate maana ya kuhudumiwa,lakini hata wale wanaotoa huduma ukimweka mahali pazuri panapovutia anapata moyo wa kutoa huduma na morali wa kazi,

“Kwa hiyo katika utawala bora tunaendelea kuboresha majengo haya,tunajenga majengo ya halmashauri,tunajenga majengo ya wakuu wa mikoa lakini zaidi ni kwamba ili haki itoke vyema hata majengo  ya mahakama tumeanza kuyaboresha .”amesema Rais Samia na kuongeza kuwa

“Utafiti unaonyesha kwamba mwanadamu akifanya kazi kwenye mazingira basi kama ni haki anakuwa ametulia ,anatoa haki ipasavyo, na kama ni huduma anatoa huduma ipasavyo na ndio maana tunatumia pesa nyingi sana kujenga majengo ya aina hii .”

Amesema,Serikali itaendelea  kujenga majengo ya aina hiyo katika mikoa mbalimbali hasa maeneo ya Makao Makuu ya Kanda.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TBA Msanifu Majengo Daud Kandoro amemshukuru Rais Samia kwa kuzindua jengo hilo na kupongeza kwa namna lilivyobuniwa na lilivyojengwa na kuonyesha ni jengo la kiwango.

Hata hivyo amesema,huo ndio wajibu wao kuhakikisha majengo yanajengwa kwa ubora unaotakiwa ili yaweze kukaa muda mrefu kwani Sereikali inatoa pesa nyingi kwa ajili ya majengo hayo.

“Sisi ni wasimamizi wa majengo ya serikali, ofisi ,nyumba za watumishi ambazo watakaa salama na kuleta tija katika kutoa huduma,lakini jengo hili ni mfano mmoja ambapo tumeshiriki tangu kufanya ubinifu hadi kujenga.”amesema Kandoro

Aidha katika ujenzi wa jengo hatua zote zimezingatiwa ili kuhakikisha linakuwa na uimara wa kutosha ambapo upimaji wa udongo ulifanyika ili kuelewa msingi gani unapaswa kujengwa lakini pia vifaa vyote vilivyotumika vimepita maabara kupimwa na kuthibitishwa kuhakikisha jengo linakuwa na ubora unaotakiwa na kuishi muda mrefu.