January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia apongezwa kwa miongozo madhubuti ya ukusanyaji wa kodi

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa miongozo yake madhubuti katika ukusanyaji wa kodi bila kutumia mabavu, akisisitiza kuwa mbinu hiyo imezaa matunda makubwa katika kuongeza mapato ya nchi.

Pongezi hizo zimetolewa Januari 23, 2025, wakati wa kilele cha Siku ya Mlipakodi, ambapo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewatunuku walipakodi 1,228 kutoka sekta mbalimbali nchini kwa mchango wao wa kikodi ambapo Rais Samia anakabidhi tuzo hizo, ikiwa ni ishara ya shukrani kwa walipakodi.

Dkt. Mwigulu amesema kauli ya Rais Samia ya kuhimiza ukusanyaji wa kodi kwa hiari imechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha makusanyo makubwa ya kodi. Pia ameeleza kuwa Rais amekuwa akifanya mapitio ya sheria za kodi kupitia tume maalum na kuwezesha TRA kujenga mifumo ya kisasa ya ukusanyaji wa kodi.

“Katika kipindi cha uongozi wa Mhe. Rais Samia, fedha nyingi zimeongezwa kwenye sekta za kilimo, huduma za jamii, afya, na miundombinu, ambapo barabara nyingi zimejengwa mijini na vijijini,” amesema Dkt. Mwigulu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema mkoa huo utaimarisha biashara za usiku na mchana ili kuchochea maendeleo. Amebainisha kuwa hatua za kufunga taa na kamera za CCTV zinaendelea kufanyika ili kuboresha usalama, huku vyombo vya dola vikiwa tayari kulinda mazingira ya kibiashara.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TRA, Mussa Uledi, amesisitiza umuhimu wa uwepo wa Rais Samia katika utoaji wa tuzo hizo, akisema kuwa uwepo huo unatoa motisha kwa walipakodi.

Uledi ameongeza kuwa TRA imeanza kutumia mfumo wa TANCIS, ambao unarahisisha shughuli za forodha bandarini, mipakani, na viwanja vya ndege, sambamba na kuhakikisha mifumo ya taasisi nyingine inasomana ili kuongeza ufanisi.