Na Jackline Martin, Timesmajiraonline, Ifakara
RAIS Samia Suluhu Hassan , ameitaka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kufika ukanda wa Kilombero kununua mpunga kwa bei ya sh. 900 kwa kilo badala ya sh. 570 wanayouza sasa ili kuwawezesha wakulima kujitegemea katika kuendesha kilimo hicho.
Rais Samia alitoa agizo hilo jana mkoani Morogoro wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Ifakara Wilaya ya Kilombero ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake Mkoani humo.
Rais Samia alisema watakarabati SKIM ya Idete ili isimame na imwagiliwe vizuri ili watu wawe na kilimo cha uhakika.
Aidha, aliuagiza uongozi wa mkoa na wilaya kusimamia wakulima wapate bei halali ili miaka ijayo waweze kujikimu wenyewe na kulima vizuri.
Pia Rais Samia aliwaagiza viongozi kuacha mara moja kunyonya nguvu za wakulima badala yake kutenda haki. “Katika biashara hii tumeweka viongozi ngazi mbalimbali muwasaidie wananchi , viongozi mnapojiingiza kwenye biashara hii mnakwenda kunyonya nguvu ya mkulima hufanyi haki, kama unafanya biashara hii ya kuongeza kipimo kwenye bishara ya mkulima na ukalipa kidogo ili wewe unufaike, haufanyi haki, kaa mara mbili na ujisikilize, mkulima anapoteza nguvu yake kubwa apate kwa jasho lake na dini zote zinatuambia hivyo kila mtu apate kwa jasho lake,” alisema.
Kadhalika, Rais Samia aliwaagiza wakulima hao wa mpunga kuhakikisha wanasambaza mchele wa Tanzania duniani kote ili kuvutia fedha za kigeni nchini .
Mbali na hayo, Rais Samia alisema Serikali imejipanga kukuza na kuendeleza sekta ya kilimo kupitia mradi wa BBT kujenga kesho bora ya vijana ili iweze kutoa ajira kwa vijana
Kwa upande wa elimu, Rais Samia aliwataka wazazi na walezi kuweka mkazo kwa kuhimiza watoto kwenda mashuleni kwani Serikali imedhidhatiti kutoa elimu bure ili kila mtoto apata elimu ya darasani.
“Kwenye masuala ya elimu nafurahi sasa Kirombelo ina shule za msingi 184, Mlimba 99, Ifakara Mjini 85 na shule za sekondari 55, Mlimba 26 na Ifakara Mjini 29 hizi ni shule nyingi sana kupitia shule hizi tumeweza kuongeza idadi ya watoto wetu wanaopata fursa ya kusoma,” alisema.
“Tumejenga shule hizi nyingi sana, lakini pia tumeondoa gharama kwa wazazi kusomesha watoto kwa jina la elimu bure, lakini elimu hii siyo bure, bali ni elimu ambayo inalipiwa na Serikali, Serikali tunalipa kwa ajili ya watoto wetu niwaombe sana wazazi wenzangu waacheni watoto wakasome madarasa haya na shule tunazozijenga, walimu tunaowaajiri ni kwa ajili ya watoto wetu hawa,” alisema na kuongeza;
“Inasikitisha unapita kwenye ziara saa za watoto kuwepo shule unakuta watoto wengi wanazubaa zubaa njiani na hawapo shule, niwaombe sana waacheni watoto waende wakasome, Serikali imeingia gharama ili watoto wetu wasome.”
Kwa upande wa VETA, Rais Samia alisema tayari Serikali imejenga VETA kila wilaya shule ambazo zinafanya elimu ya maarifa inawapa watoto amali za ujuzi zinazowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.
Kuhusu Umeme Rais Samia alisema tayari wamefikisha umeme kwenye vijiji vyote 110 vya Wilaya ya Kilombero, ambapo kazi inayofanyika ni kusambaza kwenye vitongoji na kuunganisha kwenye taasisi na nyumba za watu.
Rais Samia alisema kuongezeka kwa vituo vya afya na shule kunaleta changamoto nyingine ikiwemo ya uhaba wa watumishi, walimu na watumishi kwenye sekta ya afya, hivyo aliwahakikishia wakazi wa wilaya hiyo kwamba ndani ya mwaka huu watumishi wa afya wataajiriwa ili kuziba mapengo au kupunguza upungufu uliopo
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema tayari wametekeleza agizo la Rais Samia la kuhakikisha Mradi wa Bonde la Kilombero unaanza haraka kufanyiwa kazi, ambapo tayari mkandarasi yupo kazini.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini