January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia apeleka Bil 35 kumaliza kero ya maji Kasulu

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amepeleka kiasi cha sh bil 35 katika Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma ili kutatua kero ya maji kwa wakazi wa Wilaya hiyo.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kasulu (KUWSA) Mhandisi Athuman Kilundumya alipokuwa akiongea na Mwandishi wa gazeti hili aliyetembelea Wilaya hiyo hivi karibuni.

Amesema kuwa Halmashauri hiyo yenye wakazi 238, 321 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ni miongoni mwa Miji iliyokuwa na changamoto kubwa ya maji, hivyo serikali ya awamu ya 6 imeamua kumaliza kero hiyo.

Amebainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 serikali imepeleka kiasi cha sh bil 35 kupitia Mradi wa Miji 28 ili kuongeza uzalishaji na usambazaji maji katika Mji huo ili kuwezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama ya uhakika.

Mhandisi Kilundumya amesema kuwa hali ya upatikanaji huduma ya maji katika Mji huo ni chini ya asilimia 60 na hata maji yanayopatikana sio safi na salama hivyo ujio wa mradi huo ni mkombozi kwa wakazi wa halmashauri hiyo.

‘Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, fedha tayari zimeshafika na utekelezaji wa mradi umeanza mwezi Aprili mwaka jana na unatarajia kukamilika mwezi Novemba 2025, kazi inaendelea kwa kasi kubwa,’ ameeleza.

Ametaja shughuli ambazo zinafanyika kupitia mradi huo kuwa ni ujenzi wa chanzo (intake) chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 16 za maji kwa siku na ujenzi wa chujio lenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 15 kwa siku.

Shughuli nyingine ni ujenzi wa matenki yenye ujazo wa lita mil 2.5 moja linajengwa eneo la Kumnyika likiwa na ujazo wa lita mil 2 na lingine lenye ujazo wa lita laki 5 linajengwa eneo la Rusunwe.

Aidha wamejenga njia kuu ya bomba yenye urefu wa km 20 ambayo itapeleka maji kwenye tenki la Rusunwe na Kumnyika ili kusambaza maji hayo katika Mitaa mbalimbali ikiwemo makazi ya wananchi ili kupanua wigo wa upatikanaji maji.

Mkurugenzi amebainisha malengo makuu ya mradi huo kuwa ni kuongeza usambazaji huduma ya maji safi na salama katika halmashauri hiyo ili kuwaondolea kero iliyokuwa ikiwakabili.

Msimamizi wa mradi huo Mhandisi Goodluck Shefatia amesema kuwa awali jumla ya miradi 15 ya maji ilitekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo kisima cha Nyantare kinachozalisha lita 57,000 kwa sasa.

Mingine ni kisima cha Hwazi lita 15,000 kwa saa, kisima cha Mdyanda lita 51,000 kwa saa, kisima cha Juhudi katika kata ya Murusi lita 35,00 kwa saa huku vyanzo vya zamani vikiwa ni mto Miseno, Chai, Nyansha na Nyakatoke (chemchem).

Ameeleza kuwa vyanzo hivyo havitoshelezi mahitaji wakazi wa halmashauri hiyo hali iliyopelekea kuwepo malalamiko mengi ya wananchi, hivyo akamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwaletea kiasi hicho cha fedha ili kumaliza kero hiyo.