Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Kasulu
SERIKALI ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepeleka sh. bil 1.06 katika Kijiji cha Nyamnyusi, Kata ya Nyamnyusi Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma ili kutatua kero ya maji iliyodumu kwa miaka mingi.
Akizungumza Jana Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani humo Mhandisi Edward Kisalu alisema kuwa Kijiji hicho kilikuwa hakina huduma ya maji safi kwa miaka mingi sana.
Amebainisha kuwa tegemeo pekee kwa wakazi wa Kijiji hicho ilikuwa maji ya mito na visima vya kienyeji kwa ajili ya matumizi ya kila siku hali iliyopelekea wengi wao kupata athari za kiafya mara kwa mara ikiwemo kupoteza maisha.
“Tunamshukuru sana Rais kwa kutuletea kiasi cha sh bil 1.06 kwa ajili ya kuanza utekelezaji mradi mkubwa wa maji katika Kijiji hicho, utekelezaji mradi huu umeanza mwaka jana na unatarajia kukamilika mwakani’, amesema.
Mhandisi Kisalu alitaja kazi zilizopangwa kufanyika kwenye utekelezaji wa mradi huo kuwa ni ujenzi wa chanzo cha mradi (Mto ngaraganza), ujenzi wa tenki la lita 225,000, magati 37 na ununuzi na ulazaji bomba zenye urefu wa km 29.8.
Ameeleza kuwa mradi huo unaotekelezwa kwa fedha za programu ya PforR (Payment for Results) umeanza kutekelezwa Aprili 7, 2023 na unatarajiwa kukamilika Juni 2024 na kunufaisha zaidi wa wakazi 13,987 wa Kijiji hicho.
Ameongeza kuwa kata hiyo yenye vijiji 3 vya Nyamnyusi, Kitema na Mkiheta ni miongoni mwa kata zilizokuwa na kero kubwa ya maji lakini serikali ya Rais Samia imeendelea kupeleka fedha katika kila kata ili kutekelezwa miradi ya maji.
Baadhi ya manufaa watakayopata wakazi wa kijiji hicho kwa kutekelezwa mradi huo ni kupungua kwa maambukizi ya magonjwa yatokanayo na kunywa maji machafu na kuwapunguzia muda wa kutembea umbali mrefu kufuata maji mtoni.
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM