Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma
MABORESHO yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa kipindi cha miaka miwili yameiwezesha Serikali kuokoa sh. bilioni 195.2 ndani ya kipindi hicho, kutokana taasisi hiyo kuwa na vifaa tiba vinavyowezesha wagonjwa wengi kupatiwa huduma hapa nchini.
Fedha hizo sasa zitatumika kwa ajili ya shughuli nyingine za wakuwaletea maendeleo wananchi.
Haya yalisemwa jijiji hapa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Prof Abel Makubi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo na mafanikio ambayo yamepatikana kwa kwa kipindi cha miaka miwili.
Prof.Makubi amesema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia, MOI imeanzisha huduma mpya, kufufua na kuziimarisha kwa kufanywa na watalaamu mabingwa wa hapa nchini baada ya Serikali kutoa fedha zaidi ya sh. Bil 4.5 kwa ajili ya vifaa.
Kwa mujibu wa Profesa Makubi kiasi hicho kimeokolewa kutokana na wagonjwa wengi kupata huduma ya mifupa nchini badala ya kwenda nje ya nchi.
Amesema walifanya upasuaji wa kibingwa bobezi kwa wagonjwa 14,574 ikilinganishwa na wagonjwa 13,618 waliofanyiwa mwaka 2019/2020 hadi 2020/2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.4.
Amefafanua gharama za matibabu hayo ndani ya nchi zilikuwa sh. bilioni 36.4, na kama wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu jumla ya sh. bilioni 231.6 zingetumika , hivyo Serikali imeokoa sh. bilioni 195.2.
Ametaja huduma iliyotolewa ni huduma ya kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo kupitia tundu la pua (transsphenoidal hypophysectomy) ambapo wagonjwa 31 wameshafanyiwa upasuaji, huku gharama za upasuaji huo hapa nchini zikiwa ni sh milioni 8 hadi 16, wakati nje ya nchi ni zaidi ya sh. milioni 40.
Huduma nyingine iliyoanzishwa kwa mujibu wa Prof. Makubi ni huduma ya matibabu ya maumivu sugu ya mgongo bila ya upasuaji, ambapo tangu kuanzishwa huduma hiyo Mei 2023, tayari wagonjwa 97 wamepata huduma hiyo.
Amesema gharama za upasuaji huo hapa nchini ni sh. milioni 1 na nje ya nchi ni zaidi ya sh. milioni 9.
Nyingine ni kufufuliwa kwa huduma za Upasuaji Marudio ya vipandakizi (Revision Implant Surgery) ambapo wagonjwa 57 kwa kurekebisha nyonga na magoti kwa wagonjwa ambao walifanyiwa upasuaji kati ya miaka 15-19 iliyopita.
“Huduma hizi mpya, zimeiwezesha taasisi kupunguza kero nyingi za ucheleweshaji wa matibabu na hata wagonjwa wengine kupata madhara ya kudumu, lakini pia zimepunguza kwa kiasi kikubwa rufaa za wagonjwa nje ya nchi ambapo kwa sasa kwa magonjwa ya ubongo na mishipa ya fahamu asilimia 96 tunafanya hapa na upasuaji wa mifupa asilimia 98 tunafanya hapa,”amesema Prof.Makubi.
Aidha Prof Makubi amesema kuwa Taasisi hiyo imetumia shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ununuzi wa vipandikizi upasuaji (surgical Implants)” ili kukabiliana na changamoto la uhaba wa “implants” kwa wagonjwa ambao uliokuwa unasababisha wananchi wachelewe kupata huduma.
Amesema vifaa hivyo vimesaidia kuendelea kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa ya mifupa, ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu na hivyo kuokoa maisha ya Watanzania wengi na pesa za Serikali ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu.
Aidha, amesema taasisi imenunua vifaa vya kisasa, zikiwemo mashine za kupumulia (ICU Ventilators), Monitors, vitanda na ambulance ya kisasa vyenye thamani ya sh. billion 1.3 zilizotolewa na Serikali.
Vilevile amesema Serikali imeboresha huduma za karakana ya viungo bandia, ambapo jumla ya viungo bandia 555 vimetengenezwa.
Aidha, amesema kuwa Taasisi hiyo imeanzisha huduma mpya ya utengenezaji wa mkono wa umeme ambapo tayari wagonjwa 5 wameshahudumiwa, gharama zake ndani ya nchi ni zikiwa ni sh milioni 15 na nje ya nchi ni milioni 30 hadi 60.
Amefafanua kuwa Serikali ya Rais Samia imeendelea kuhudumia wananchi wasiokuwa na uwezo, ambapo kupitia MOI ilitoa misahama yenye gharama ya sh. bilioni 6.5 kwa miaka miwili.
Pamoja na hayo amesema katika Mipango yao ya utekelezaji wa Bajeti ya Fedha ya Mwaka 2023/24, Serikali imetenga jumla ya sh. bilioni 55.9 kwa MOI ili kuboresha huduma za Tiba na shughuli za uendeshaji.Mwisho
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa