January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia amaliza kero ya huduma za Afya Ilege

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Kaliua

SERIKALI ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imemaliza kero ya upatikanaji huduma za afya kwa wakazi wa Kata ya Ilege, Wilayani Kaliua Mkoani Tabora baada ya kuwajengea Kituo kipya cha afya.

Akizungumza na Mwandishi wa gazeti hili jana diwani wa Kata hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Japhael Lufungija alisema kuwa Rais Samia amewapatia zaidi ya sh mil 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo hicho.

Alibainisha kuwa mradi huo ambao umetekelezwa kwa awamu mbili sasa hivi umekamilika kwa asilimia 100 na unatoa huduma za afya kwa makundi yote ikiwemo akinamama wajawazito na huduma za kliniki kwa watoto wote.

Lufungija alifafanua kuwa mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2022/2023 hadi kukamilika umegharimu kiasi cha sh mil 546.5 ambapo sh mil 500 zilitolewa na serikali kuu kupitia fedha za tozo na kiasi cha sh mil 46.5 ni mapato ya ndani.

‘Tunamshukuru sana Mama yetu kwa kujali maisha ya wananchi na kutuletea kiasi hicho cha fedha, hakika mama amesikia kilio chetu, akinamama walikuwa wanatembea zaidi ya km 10 kufuata huduma hizo kata nyingine’, alisema.  

Mwenyekiti alifafanua kuwa awamu ya kwanza walipokea sh mil 250 na wakazi wa Kata hiyo wakajitolea mawe yenye thamani ya sh mil 3, fedha hizo zilitumika kujenga majengo 3 ya OPD (wagonjwa wa nje), maabara na kichomea taka.

Kwa awamu ya pili alisema walipokea sh mil 296.5 ambapo sh mil 250 zilitoka serikali kuu na sh mil 46.5 ni za mapato ya ndani ya halmashauri ambapo fedha hizo zilitumika kujenga jengo la wazazi, upasuaji na nyumba 1 ya mtumishi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt Rashid Chuachua aliwataka wakazi wa kata hiyo kwenda kupata matibabu katika Kituo hicho na kuacha kutumia dawa za kienyeji kwa kuwa hazina uthibitisho wowote wa kitaalamu.

Alisisitiza kuwa serikali ya awamu ya 6 ina dhamira ya dhati ya kumaliza kero zote zinawakabili wananchi katika sekta zote hivyo akawataka kumwamini na kuunga mkono juhudi zake kwa kutunza miundombinu ya miradi inayotekelezwa.

Mtendaji wa Kata hiyo Aliamin Athuman alisema kuwa mradi huo ni mkombozi kwa wananchi kwani wengi wao walikuwa wanapata shida sana kwa kufuata matibabu katika kata nyingine, wengine walipoteza maisha kutokana na umbali.