Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Dodoma
BENKI ya NMB imepandisha kiwango cha mikopo kwa wakulima na wafugaji kutoka Shilingi Bilioni 730 mwaka 2021 hadi Shilingi Trilioni 1.6 mwaka huu 2024 huku ikiweka mkakati wa kuinua sekta hiyo.
Kutolewa kwa mikopo hiyo kumesaidia kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji kwani kiasi cha Shilingi bilioni 505 ni mikopo ya wafugaji kwa lengo la kunenepesha mifugo na kuboresha maeneo ya malisho kwa kundi hilo.
Akizungumza mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan leo Agost 8,2024, Mtendaji Mkuu wa NMB Ruth Zaipuna amesema kutolewa kwa mikopo hiyo ni sehemu ya mkakati wa benki katika kuunga mkono sera nzuri za Serikali ya awamu ya sita.
Takwimu hizo zimemfurahisha Rais Dk Samia Suluhu Hassan na akiwa kwenye banda la maonyesho la NMB amesema ‘Kazi Iendelee’ kauli ambayo huitumia anapokubaliana na jambo hasa kwenye miradi ya maendeleo.
“Mheshimiwa Rais tunakupongeza sana katika maoni yako hasa ya kuwainua wakulima na wafugaji nchini, na sisi NMB tunayo mikakati ya kusaidia sekta ya kilimo na mifugo ambako tumeona kuna mapinduzi makubwa,” amesema Zaipuna.
Mtendaji Mkuu ameeleza kuwa kati ya mikopo iliyotolewa,Shilingi bilioni 450 zimetolewa kwenye mpango wa riba nafuu ya asilimia 9 ambako ndiko waliko wakulima na wafugaji.
Zaipuna amesema benki hiyo imeanzisha mkakati maalumu wa kuwafikia wakulima na wananchi kupitia mpango wake wa kufungua akaunti za Shilingi 1000 ambako mamilioni ya Watanzania wamejiunga huko hivyo kuwawezesha wananchi kupata mikopo kwa urahisi.
“Mheshimiwa Rais akaunti hii imerahisisha wananchi na wakulima kupata mikopo kwa njia ya mtandao (Mkopo fasta) bila kuweka foleni benki na mikopo hiyo inaanzia kiasi cha Shilingi 1000 hadi Shilingi milioni moja,” amesema.
Kiongozi huyo amemwambia Rais kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kukuza maono na wametumia maonyesho ya wakulima Nane Nane kutoa elimu ya fedha ambako wananchi wamekuwa na mwitikio mkubwa.
More Stories
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya
Prof.Muhongo awapongeza vijana 32 waliotembea kwa miguu kutoka Butiama hadi Mwanza
Rais Samia atimiza ahadi Hanang