*Asema asikilizi kelele, anachotaka ni mageuzi ya kiuchumi, atakayetaka kumkera akanyage uchumi, asena hatayumbishwa na maneno
Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Dar
RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema kazi aliyopewa na Watanzania amesimama na anaifanya na amejigeuza chura asikilizi kelele, bali anachotaka ni megeuzi ya kiuchumi.
Rais Samia alitoa kauli hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya kupokea gawio na michango kutoka mashirika na taasisi 10 za umma.
“Kelele nyingi zinapigwa, wakiona kimya wanaona wanitukane kama nitajibu, sijibu. Ninachotaka ni mageuzi ya kiuchumi katika nchi hii sasa kwenye hayo mageuzi kuna watakaoumia,” alisema Rais Samia na kuongeza;
“Anayetaka kunikera mimi anikanyagie uchumi wangu, katika mageuzi haya tutawakanyaga wengi wale ambao hawataki kwenda mbele na ndiyo hao watakaopiga kelele.”
Rais Samia amesema hatakuwa na uvumilivu kwa mashirika ya Serikali ambayo yamebweteka yakisubiri msaada kutoka serikalini.
Rais Samia amesisitiza kwamba ataendelea kusimamia na kufuatilia kwa ukaribu ajenda ya mabadiliko katika mashirika ya umma.
Amesema kamwe hatayumbishwa na maneno yanayolenga kumtoa kwenye reli. Katika kutekeleza ajenda hiyo na amemwelekeza Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu kusimama imara kuhakikisha mageuzi hayo yanafanikiwa na kuleta tija kiuchumi.
Amesema Tanzania haina budi kufanya mageuzi ya kiuchumi na mchakato wa kufanya mageuzi hayo ni lazima uhusishe mashirika na taasisi za umma.
Rais Samia ametoa mfano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ambayo imetoa gawio la sh. bilioni 153.9 akisema mafanikio hayo ni matokeo ya uwekezaji uliofanyika bandarini ambako kuna wawekezaji wawili.
“Pale TPA mwaka jana kiwango hakikuwa hiki, lakini kwa mageuzi makubwa yaliyofanyika bandarini mwakani tunatarajia makubwa zaidi,” amesema.
“Pale bandarini kuna watu wawili, hivyo tunatarajia makubwa. Wale waliopiga kelele mama kauza bandari, mara kauza bahari mauzo yale faida yake ni hii leo, huu ni mwanzo tunatarajia kupata makubwa zaidi kwa bandari zote,” amesema.
Rais Samia pia, ameonesha kutoridhishwa na utendaji wa mashirika yanayomilikiwa na Serikali, akimtaka Msajili wa Hazina kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kunakuwa na matokeo chanya.
“Mchechu fanya kazi yako najua utalaumiwa lakini hiyo ndiyo kazi niliyokupa simama ifanye mimi kazi niliyopewa na Watanzania nimesimama naifanya na mnashuhudia matusi ninayotukanwa mpuuzi, hana maana, huyu bibi, yaani mambo tele lakini najigeuza chura,” amesema.
Katika hatua nyingine Rais Samia amengaza vita mageuzi ya kiuchumi akiyataka mashirika hayo yakajifunze kutoka kwenye mashirika ambayo Serikali imeingia ubia na sekta binafsi.
“Kampuni zilizotoa gawio ni zile ambazo Serikali ina hisa chache kwa maana hisa nyingi ni za sekta binafsi, zile za Serikali hazipo hapa lakini sera ni zile zile ila kampuni zetu zimebweteka.
Sekta binafsi wanahangaika kwa kutumia mbinu zote za biashara ili waweze kupata faida, hapa kuna somo kwa mashirika yetu,” alisema na kuongeza;
“Lengo kwenye gawio ni asilimia 11 lakini tupo asilimia tatu ambayo tulikuwa nayo mwaka jana, ni imani yangu kuwa mwakani tutasogea. Tutasogea endapo mashirika 159 ambayo hayakutoa gawio mwaka huu nayo yatajituma kufanya kazi yaweze kuchangia Serikali,” amesema.
More Stories
Maandalizi ya mkutano mkuu CCM yapamba moto
Walimu S/ Sekondari Ilala wafundwa juu ya maadili ya wanafunzi
Dkt. Samia afungua skuli ya sekondari Misufini, Bumbwini