December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia afanya teuzi mbalimbali

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

RAIS Samia Suluhu Hassan amemteua Profesa Masoud Muruke kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), akichukua nafasi ya Profesa Willy Komba aliyemaliza muda wake.

Profesa Komba ameiongoza TSC tangu Juni 2020 na wadhifa wake umekoma jana , Mei 15, 2024, baada ya muda wake wa utumishi ndani ya TSC kumalizika.

Taarifa ya uteuzi wa Profesa Muruke imetolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus.  Rais Samia yupo Ufaransa kushiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Afrika uliofanyika nchini humo

Katika uteuzi huo, wengine walioteuliwa kwa mujibu wa taarifa hiyo ni Ishmael Kasekwa anayeenda kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

 Kasekwa ameteuliwa kushika wadhifa huo kwa kipindi cha pili, baada ya kumaliza muda wake wa awali.

Sambamba na hao, Rais Samia pia amemteua Balozi Maimuna Tarishi kuwa mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.

Balozi Tarishi anarithi mikoba kutoka kwa Profesa Joseph Bucheishaija aliyemaliza muda wake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, Rais Samia pia amemteua Martin Kilimba kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Biashara Tanzania (TCB).

Kilimba anaenda kuchukua nafasi ya Dk Edmund Mndolwa, mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi, ambaye muda wake umemalizika.