January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia aboresha zaidi sekta ya mifugo.

Na Mwandishi wetu,TimesMajira online

Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeahidi kuboresha zaidi sekta ya mifugo kupitia njia mbalimbali.

Naibu Waziri wa Uvuvi na Mifugo Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amebainisha hayo (22.02.2023) katika Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi madume ya ng’ombe 36 aina ya boran Heifer kwa halmashauri ya Buchosa.

Mhe. Ulega amesema lengo la serikali ni kuona vijana wanafanya uzalishaji wa mali kwa kuingia katika sekta ya mifugo na kupeleka mifugo hiyo sokoni.

‘’Nchi yetu ina ng’ombe milioni 33 na bado tija ipo chini sana kutokana na viwanda vingi havipati malighafi ya kutosha. Mifugo inatakiwa kuongeza tija na pato la taifa na kwa mtu mmoja mmoja’’ Amesema Mhe. Ulega.

Ameongeza kuwa kupitia programu maalum ya Samia Ufugaji kwa Tija (SAUTI), serikali imefanikisha kuanzisha mafunzo ya unenepeshaji mifugo ambapo takriban vijana 70 wanapatiwa mafunzo hayo kwa vitendo katika Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Wilayani Misungwi.

Mhe. Ulega amesema anamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya mageuzi kwenye Sekta ya Mifugo.

Aidha amesema serikali imeanzisha vituo atamizi vya SAUTI ambapo mpaka sasa kuna vituo nane kwa ajili ya vijana kufunzwa.
 
Amesema pia kupitia vituo hivyo atamizi vijana watafundishwa namna bora na kisasa ya kutengeneza mashamba ya malisho na upatikanaji wa mifugo bora.
 
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga aliishukuru serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipata ng’ombe kwa halmashauri ya Buchosa.

Naye mmoja wa wanafunzi hao ameishukuru serikali kwa kuja na programu hiyo ya ufugaji ambayo itawasaidia kupata ajira.