*Ni ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake atunukiwa tano, Chuo Kikuu cha Korea nacho chajitosa chasema anatoa somo kubwa kwa vizazi vijavyo.
Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar
RAIS Samia Suluhu Hassan, ameandika rekodi ambapo ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, ametunukiwa Shahada za Udaktari wa Heshima (PhD) tano kutoka vyuo vikuu viwili vya ndani ya nchi na vitatu nje ya nchi.
Rais Samia ametimiza Shahada ya Tano ya Udaktari wa Heshima baada ya jana kutunukiwa PhD hiyo na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea (KAU) kutokana na mchango wake katika sekta ya usafiri wa anga.
Rais Samia ametunukiwa shahada hiyo jijini Seoul, Korea Kusini anakoendelea na ziara yake ya kikazi ya siku saba, ambapo ameshiriki shughuli mbalimbali ikiwemo yeye na mwenyeji wake, Rais wa Korea Yoon Suk Yeol.
Miongoni mwa shughuli hizo ni pamoja na kushuhudia utiaji saini wa mkataba mmoja, Hati za Makubaliano (MOU) mbili na Tamko la Pamoja la kuanzisha Mkataba wa Ushirikiano wa Uchumi (EPA).
Mkataba huu utaiwezesha Tanzania kupokea mkopo kutoka Korea wa kiasi cha Dola za Kimarekani Bilioni 2.5 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia (2024- 2028).
Fedha hizo ni kwa ajili ya miradi ya miundombinu ya maendeleo zinatolewa chini ya Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi wa Serikali ya Korea (EDCF).
Uamuzi huo wa kumtunuku Rais Samia PhD ya heshima kutoka Chuo Kikuu cha KAU umetokana na mchango wake katika sekta ya usafiri wa anga nchini.
Hiyo ni kutokana na hatua alizochukua hasa wakati na baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19 kama vile kuongeza safari za ndege na ndege katika Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL).
Akizungumza baada ya kutunukiwa udaktari wa heshima, Rais Samia alishukuru Chuo hicho na kueleza kwamba sekta ya usafiri wa anga imekuwa na umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi.
Kutokana na umuhimu huo, Rais Samia alisema ana nia ya kujenga chuo cha masuala ya anga nchini kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea.
Amesema ilikuwa ni muhimu kulihuisha Shirika la ATCL na tangu hatua hizo zilipoanza kuchukuliwa, mapato ya ATCL yameongezeka kutoka sh. bilioni 33 mwaka 2016/17 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 308.4 mwaka 2023.
Kwa mujibu wa Rais Samia safari za ndege za kimataifa pia zimeongezeka kutoka 26 mwaka 2016/17 hadi kufikia 33 mwaka 2021 na hivyo kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini hadi kufikia karibu watalii milioni mbili wanaotembelea Tanzania.
“Ni muhimu kutambua kwamba waendeshaji wa ndani na wasafiri wamekuwa sehemu ya sekta hii kwani takwimu zinaonyesha pia idadi ya wasafiri imeongezeka kwa asilimia 25.6 kutoka abiria milioni tatu kabla a mlipuko wa Uviko-19 hadi abiria milioni 3.8 kufikia mwaka 2023,” alisema.
Rais Samia amesema mwaka 2006, Tanzania ilikuwa na ndege moja pekee, lakini hadi sasa ina ndege 14 za abiria pamoja na ndege moja ya mizigo. Pia, amesema imeweza kupanua masafa yake kutoka mataifa manne hadi kufikia mataifa 24.
Pia soko la shirika la ATCL la safari za ndani limefika asilimia 53 asilimia kutoka asilimia 2.4 tu mwaka 2022/23, huku idadi ya abiria imeongezeka kwa asilimia 42 kutoka milioni 4.8 mwaka 2015 hadi milioni 6.8 mwaka 2024.
Mbali na hapo, idadi ya marubani waliosajiliwa na wahandisi wa ndege imeongezeka kufikia 604 ikiwa ni ongezeko la asilimia 21 na wahandisi kufikia 76 ambalo ni ongezeko la asilimia 181 mpaka mwisho wa mwaka 2023.
Kwa upande wake Rais wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea, Hee Young Hurr, amesema chuo hicho kina historia ya miaka 72 na kimekuwa na ushirikiano na Tanzania hasa kwenye udhamini wa masomo ya shahada ya umahiri.
Amesema huo ni mwanzo mzuri wa ushirikiano kati ya Tanzania na Korea. “Uongozi wako unavutia na tumeamua kukutunukia shahada ya udaktari katika usimamizi wa usafiri wa anga,” alisema Hurr.
Mwenyekiti wa Bodi ya KAU, Amidi wa Shule Kuu, Soo Chang Hwang alisema kama kiongozi mwanamke, anatoa somo kubwa kwa vizazi vijavyo.
Amesema uongozi wake katika sekta ya anga ni wa kipekee na umekuwa na manufaa makubwa ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya ndege zinazotua nchini, kuongezeka kwa idadi ya ndege za ATCL pamoja na mapato.
Amesema kwa kwa niaba ya Bodi ya KAU, tunakupongeza na shahada hii ni ishara ya heshima kwako kwa kile unachokifanya na tunatarajia utaendelea kuwa na ushirikiano na Chuo chetu,” alisema Hwang.
Rais Samia leo anatarajiwa kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kati ya Korea na Afrika.
Mbali na Chuo cha KAU, akiwa na miaka mitatu pekee, tayari ametunukiwa Shahada nne za Heshima (Honoris Causa)
Kilianza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambacho Novemba 30, 2022 kilimtunuku Shahada ya Juu ya Heshima kwenye Humanitia na Sayansi Jamii (Social sciences), Oktoba 10, 2023 kikafuatia Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha nchini India na Desemba 28, 2023 Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) kumtunuku Shahada nyingine ya Uzamivu ya Usimamizi wa Utalii na Masoko (Doctor of Philosophy in Tourism Management and Marketing- Honors Causa).
Shahada ya Heshima ya Falsafa ni Shahada ya Juu sana katika elimu inayotolewa na Taasisi ya Elimu ya Juu (Chuo Kikuu) bila ya kumhitaji Mtunukiwa wa Shahada hiyo kufuata utaratibu wa kawaida na uliozoeleka wa kupata Shahada.
Utaratibu wa kawaida kupata Shahada ni mtu kuingia darasani kwa muda wa miaka fulani akisoma na kupikwa na baadae akifaulu hutunukiwa Shahada hiyo. Lakini, Shahada hii haimhitaji Mtunukiwa kuingia darasani.
Hii ni Shahada inayotunukiwa ama kutolewa kwa mtu aliyefanya jambo kubwa, la muhimu na lililoacha alama na kubadilisha maisha ya watu kwenye jamii ama Taifa.
Jambo hilo linaweza kuwa kwenye sekta ya elimu, kutumia maarifa yake kutatua changamoto kwenye jamii, kulinda na kupigania haki za binadamu.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu