January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Mwinyi:Uchumi wa bluu kuipaisha Zanzibar

Na Mwandishi Maalum, TimesMajira Online,Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameahidi kuijenga Zanzibar mpya kwa kupitia uchumi wa kisasa wa Buluu (Blue Economy).

Ahadi hiyo aliitoa katika hotuba yake ya uzinduzi wa Baraza la 10 la Wawakilishi lililofanyika huko katika ukumbi wa baraza hilo Chukwani, nje kidogo ya Jiji la Zanzibar.

Hafla ambayo ilihudhuriwa na viongozi kadhaa akiwemo Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzzibar, Amani Abeid Karume, Dkt.Ali Mohammed Shein, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Mama Maryam Mwinyi, wake wa Marais wastaafu, mabalozi na viongozi wengineo.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dkt. Hussein amesema kuwa, moja ya ahadi yake kubwa aliyoitoa kwa wananchi na ambayo imeelezwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kujenga uchumi wa kisasa wa Buluu.

Amesema kuwa Uchumi wa Buluu ama uchumi wa bahari unafungamanisha kwa pamoja sekta za uvuvi, ufugaji samaki, ujenzi wa viwanda vya samaki, ukulima wa mwani, uchimbaji wa mafuta na gesi, matumizi bora ya rasilimali mbali mbali za bahari pamoja na shughuli za utalii wa fukwe na michezo ya baharini.

Ameongeza kuwa, uchumi wa Buluu haukamiliki bila ya kuwepo kwa Bandari za kisasa zenye ufanisi wa hali ya juu.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dkt.Hussein Mwinyi ameeleza kuwa, miongoni mwa mambo yanayodhoofisha misingi ya utawala bora ni vitendo vya rushwa, uzembe, kukosa uwajibikaji, kutofuata sheria na kukiukwa kwa maadili hivyo, alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane itakabiliana ipasavyo na vitendo vyote vinavyoathiri utekelezaji wa misingi ya utawala bora.

Rais Dkt.Hussein alirejea ahadi yake kwa wananchi mbele ya baraza hilo kwamba atapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi wala kuoneana muhali na kuwaomba Wawakilishi na wananchi wote wamuunge mkono wakati wa mapambano hayo.

“Tutashinda vita hii endapo wananchi pia watatuunga mkono. Sina shaka kuwa kwa vile wao, kwa wingi wao, wanachukia rushwa na ufisadi, watakuwa tayari kutoa ushirikiano wao katika mapambano haya. Ni matumaini yangu pia vyombo husika katika jambo hili vitatekeleza wajibu wao,”amesema Rais Mwinyi.

Katika hotuba hiyo pia, Rais Dkt.Hussein alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa Chama cha ACT Wazalendo, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia kifo cha Marehemu Abubakar Khamis Bakari ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Katiba na Sheria katika Serikali ya Awamu ya Saba kipindi cha kwanza.

Rais Dkt.Mwinyi ameweka wazi kuwa kiongozi yoyote atakayemteua kwa mamlaka aliyonayo kikatiba, atamuwajibisha mara moja pindi tu akibaini na kujiridhisha kuwa anajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi.

Ameongeza kuwa, uteuzi wa viongozi na watendaji katika serikali yake utazingatia uwezo wa mtu kitaaluma, uwajibikaji na uaminifu.

Ameeleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Nane itasimamia kwa umakini nidhamu na uwajibikaji wa watumishi wa umma na haitakuwa na muhali kwa mtendaji yoyote ambae hatowajibika katika utekelezaji wa majukumu yake.

Ameongeza kuwa, atakayeshindwa kuwajibika aelewe kuwa atawajibishwa kwani uzembe na ukosefu wa nidhamu kazini huzorotesha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kwa hivyo, tabia hiyo hatoivumilia.

Amewataka viongozi wote atakaowateua katika nafasi mbalimbali wawe wabunifu na waweze kuishauri Serikali juu ya masuala yanayohusu fani na utaalamu wao huku akisisiza kwamba Serikali haitowavumilia viongozi wenye kusubiri kuambiwa kutoka kwake au Serikalini nini wafanye katika kutekeleza majukumu yao.

Akieleza kuhusu sekta ya mafuta na gesi, Rais Dkt.Mwinyi amesema kwamba, Serikali ya Awamu ya Nane itaziimarisha na kuzijengea uwezo wa kitaaluma na nguvu kazi Kampuni ya Mafuta Zanzibar (ZPDC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Mafuta na Gesi (ZPRA) ili ziweze kuiongoza sekta hiyo muhimu.

Vile vile, Rais Dkt.Hussein alisema kwamba, Serikali itaendelea kushirikiana na kampuni mbalimbali zenye dhamira njema ya kuwekeza hapa nchini katika sekta hiyo.

Aidha, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane ina malengo ya kujenga bandari kubwa ya kisasa katika maeneo ya Mangapwani itakayokuwa na sehemu kadhaa za kutolea huduma zikiwemo sehemu za kuhudumia meli zitakazobeba mafuta na gesi, chelezo kwa ajili ya matengenezo ya meli, eneo la kuhudumia meli zinazobeba mizigo na makontena, bandari ya uvuvi pamoja na bandari ya meli za kitalii.

Amegusia kuwepo kwa malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu kucheleweshwa mizigo yao bandarini na msongamano wa makontena katika Bandari ya Malindi, vitendo vya rushwa na kukosa uwajibikaji kwa baadhi ya watumishi wa bandarini.

Ameeleza dhamira ya Serikali ya kuimarisha bandari za Wete na Shumba Mjini na kuendelea na matayarisho ya ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi huko Mangapwani na kuiimarisha bandari ya Mkoani ili iweze kuhudumia meli kubwa kutoka nje moja kwa moja kwa lengo la kunyanyua uchumi na biashara kwa kisiwa cha Pemba.

Amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Nane itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha kwamba kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki.

“Tutahakikisha kwamba kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Tutaziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi,”amesema Rais Mwinyi.

Aidha, meisema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane, itaweka mazingira mazuri ya uwekezaji na uendeshaji wa biashara ili sekta hizo ziwe na mchango mkubwa zaidi katika kukuza ajira na katika Pato la Taifa.

“Ushirikiano na umoja wetu ndio utakaotuwezesha kutekeleza miradi yenye tija ikiwemo uendelezaji wa viwanda, utaliii na uchumi wa buluu; ili kufanikisha azma hii, serikali itaweka mifumo rafiki kwa sekta binafsi kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi,”amesisitiza Dkt.Hussein.

Ameongeza kuwa, Serikali itaweka mazingira rafiki kwa Wanadiaspora kuja kuwekeza nyumbani kwa lengo la kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi yanayokusudiwa kufanywa.

Kutokana na kuendelea kuimarika kwa sekta ya utalii, Rais Dkt.Hussein alisema kuwa, kunampa matumaini kwamba malengo yaliyowekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya kuongeza idadi ya wageni wanaoitembelea Zanzibar kutoka 538,264 mwaka 2019 hadi kufikia wageni 850,000 mwaka 2025 yatafikiwa.

Amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Nane itaendeleza dhamira njema ya kukuza sekta za Biashara na Viwanda hapa Zanzibar, ili kuwaletea wananchi wake maendeleo zaidi ya kiuchumi.