Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Kampuni ya Airpay Tanzania kwa kudhamini Tamasha la pili la Fahari ya Zanzibar lenye lengo la kuwawezesha wananchi kupata mikopo, mafunzo ya ujasilimali kwa njia ya kidigitali.
Rais Mwinyi ametoa pongezi hizo leo visiwani Zanzibar wakati akifungua tamasha hilo lililoandaliwa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA) chini ya ufadhili wa Airpay na kuwakutanisha zaidi ya wajasiriamali zaidi ya 200 huko Nyamanzi Mkoa wa Mjini Magharib Unguja.
Amesema anaipongeza Airpay na wadhamini wengine waliofanikisha tamasha hilo na kwamba katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 serikali imetenga bajeti ya Sh. Bilioni 41.6 kwa lengo la kuongeza nguvu katika utekelezaji wa dhamira ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.
“ZEEA tangu kuanzishwa kwake katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili imewezesha upatikanaji wa mitaji pamoja na kuimarika kwa marejesho sambamba na utoaji wa mafunzo kwa wajasiriamali pamoja kuwaunganisha na masoko ya ndani nan je ya nchi,” amesema Rais Mwinyi
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Airpay Tanzania, Yasmin Chali amesema Airpay kwa kushirikiana na ZEEA imeanzisha mfumo maalumu utakaowasaidia wajasiriamali kupata mikopo kidigitali kwa muda mfupi na rahisi.
Chali amesema kwa sasa wajasiriamali wataondokana kujaza makaratisi kwa ajili ya kuomba mikopo na badala yake watatumia simu zao ama mtandao kwa ajili ya kuomba mkopo ili kukuza na kuboresha biashara zao
“Mfumo huu utawafikia wajasiriamali wengi zaidi hivyo niwaombe wafanyabishara wote kuutumia ili kupata mikopo kwa ajili ya kuendesha biashara zao, tutatoa elimu na mafunzo mbalimbali kwa walengo ili waweze kutumia bila kikwazo cha aina yeyote ile,” amesena
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji ZEEA, Juma Burhan amesema wakala huo utaendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuweka mazingira rafiki ili kufikia lengo la kupunguza umaskini kwa wananchi wa Zanzibar.
Amesema wakala kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kutoa mikopo kwa wajasiriamali katika wilaya zote za unguja na Pemba ili kukuza mitaji ya kuendesha biashara zao.
More Stories
Vikundi Ileje vyakabidhiwa mikopo ya asilimia 10, DC Mgomi avipa somo
Wananchi Tandale wahimizwa kuchagua viongozi sahihi
Samia atua Kariakoo, ashuhudia yaliyojiri