Na Zena Mohamed,Dodoma
RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaunga mkono juhudi za wanaushirika kuanzisha Benki ya Ushirika ya Taifa kwa kuchangia shilingi bilioni 5 kama mtaji ili kuwezesha shughuli za Benki hiyo kuanza.
Pia amevitaka Vyama vya Ushirika kutokuwa sehemu ya kumnyonya mwanaushirika bali viwe mstari wa mbele kuwalinda na kuwatetea.
Amesema hayo jijini hapa Agosti 10,2024,Ikulu Chamwino,Dodoma alikutana na kuzungumza na Maafisa Ugani na wanaushirika ambapo alivielekeza vyama vya ushirika kuwa chachu ya mabadiliko na vyenye kuleta mageuzi ya fikra ikiwemo kuchangia maendeleo mapana kwa kuhamasisha wanaushirika waweze kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii na Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote.
“Serikali inadhamira ya kurudisha hadhi ya ushirika hususan ushirika wa mazao hivyo nataka ushirika uendeshwe kisasa,uwekezaji ufanywe kitaalam na ukiwa na lengo la kumnufaisha mwana ushirika moja kwa moja,”amesema Dkt.Samia.
Hivyo ameiagiza Wizara ya Kilimo kuisimamia kwa ukaribu sekta ya Ushirika ili uwekezaji unaofanywa na serikali kwenye sekta ya kilimo,mifugo na uvuvi uweze kufanywa na Vyama Vya Ushirika.
Aidha amewaagiza Maafisa Ugani na Maafisa Ushirika kuhakikisha kuwa ruzuku ya pembejeo inayotolewa na serikali inaleta matokeao makubwa zaidi,kuwafikia wananchi vijijini pamoja na kuwaelimisha mbinu bora za kilimo,ufugaji na uvuvi.
Vilevile Dkt.Samia ameitaka Wizara ya Kilimo kuandaa utaratibu wa kuwapima Maafisa ugani kwa tija inayozalishwa kwenye Kata au Kijiji nachokisimamia ili uwekezaji unaofanywa na serikali utoe matokeo tarajiwa .
Pia amewataka Maafisa ugani katika ngazi ya Kata kukaa kwenye vituo vyao na kutumia usafiri ambao serikali imewapatia kuwafikia na kuwahudumia wananchi.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito