Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline Korogwe
NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amevunja rekodi kwa kupeleka fedha nyingi kwenye miradi ya maji kwa kulenga kumtua mwanamke ndoo kichwani kwa kusogeza huduma ya maji karibu na wananchi.
Ameyasema hayo Juni 23, 2024 alipofika Kijiji cha Sisi kwa Sisi kwa ajili ya kuweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji Sisi kwa Sisi, Kata ya Hale, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
“Katika kipindi ambacho Tanzania imevunja rekodi kwa kushusha fedha nyingi sana mpaka vijijini ni kipindi cha Dkt.Samia Katika kipindi ambacho Serikali na Watanzania wako salama ni kipindi hiki ambacho mama yetu Dkt.Samia ametutendea haki wanasiasa, ametutendea haki Watanzania hivyo tunaendelea kujivunia.
“Haya yote yanayowezekana sasa yanatupa nguvu ya kufika kwenye miradi kama tusingekuwa na fedha tusingeweza kuja na kufuatilia na kuweka jiwe la msingi katika miradi mbalimbali ni kwa sababu hiyo mheshimiwa Rais amejipambanua amehakikisha kwamba anatafuta fedha za kutosha ili tuendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi ili watanzania waone matokeo kwa vitendo” amesema Mhandisi Mathew.
Mhandisi Mathew amesema yeye na wasaidizi wake kwenye Sekta ya Maji watahakikisha wanatekeleza miradi yote kwa weledi ili yale malengo ya kufikisha maji kwa wananchi yanatimia.
Kwenye taarifa ya Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa, Mradi wa Maji Sisi kwa Sisi ulianza kutekelezwa Mei 19, 2022 kwa kutumia Mkandarasi M/s DASKA INVESTIMENT LIMITED wa Mugumu, Serengeti.
Lengo la mradi huo ni kutekeleza adhma ya Serikali ya kuondoa kero ya maji kwa wananchi wapatao 1,035 wa Kijiji cha Sisi kwa Sisi katika Kata ya Hale hadi sasa mradi huo umetekelezwa kwa asilimia 98 na unakusudiwa kukamilika Juni 30, 2024 ingawa wananchi wameanza kupata huduma ya maji kwa majaribio.
Taarifa hiyo inaonesha gharama ya mradi huo hadi kukamilika kwake ni sh. 327,166,478 kupitia Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF), ambapo Mkandarasi ameshalipwa sh. 205,040,340 sawa na asilimia 62.7.
“Kazi zilizopangwa na kutekelezwa katika mradi huu ni pamoja na kufunga mitambo ya kusukuma maji. (Water pump & motor) kwa asilimia 99, ujenzi wa tanki la ujazo wa lita 75,000 kwa asilimia 97, uchimbaji wa mtaro na kufunga mabomba umbali wa mita 5,850 wenye vipenyo vya 3’’, 2.5”, 2’’ ,1.5’’ na 1’’ kwa asilimia 99, ujenzi wa vilula (DPs) sita vya kuchotea maji kwa asilimia 99, ujenzi na usimikaji wa alama za njia ya bomba 90 kwa asilimia 99, na ujenzi wa valvu chemba 12 kwa asilimia 98” ilisema taarifa hiyo.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba