November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt.Samia atarajiwa kushiriki ibada ya kumbukumbu ya miaka 40 ya Hayati Sokoine

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

FAMILI ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Hayati Edward Sokoine wanatarajia kufanya ibada maalumu ya kumbukizi ya miaka 40 ya kifo chake huku Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kushiriki ibada hiyo.

Hayo yamesemwa jiiiji hapa leo,Machi 28,2024 na msemaji wa familia hiyo,Lembris Kipuyo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio wa ibada hiyo ambapo amesema itafanyika siku ya Ijumaa,Aprili 12 mwaka huu katika kijiii cha Enguik,Monduli Juu Mkoani Arusha.

“Ibada hiyo imeandaliwa na familia ikishirikiana na Taasisi ya Hayati Edward Moringe Sokoine na itawashirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,”amesema Kipuyo

Kipuyo ameeleza kuwa Hayati Sokoine alikuwa mzalendo wa kweli, alipenda taifa lake na wananchi wake, alihakikisha kwamba rasilimali za nchi zinatumika na watanzania wote, aliwatumikia wananchi bila kubagua na alikuwa na hofu ya Mungu katika kufanya kazi zake.

Hivyo ilianzishwa Taasisi ya Hayati Edward Moringe Sokoine,ikiwa na lengo la kuenzi mema aliyoyafanya, kwani aliacha alama kubwa ambayo taifa linamkumbuka hadi leo.

Amesema Taasisi hiyo imejikita katika masuala ya elimu, kilimo, hifadhi ya mazingira, vyanzo vya maji pamoja na afya.

Akitoa historia ya Hayati Sokoine, Kipuyo ameeleza kuwa alizaliwa Agosti,1, 1938,katika kijiji cha Enguik, Monduli Juu, wilayani Monduli mkoani Arusha.

Hayati Sokoine alipata elimu ya msingi na sekondari huko Monduli na baadaye Umbwe, mkoani Kilimanjaro.

Alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vipindi viwili.

Mwaka 1961 alijiunga na chama kilichoipatia uhuru Tanganyika, Tanzania African National Union (TANU).

“Baadaye mwaka 1962 alikwenda nchini Ujerumani (wakati huo Ujerumani Mashariki) kupata masomo ya utawala hadi mwaka 1963,baada ya kurejea aliteuliwa kuwa Afisa Mtendaji wa Wilaya (sawa na Mkurugenzi wa Halmashauri hivi leo) wa Wilaya ya Masai iliyojumuisha wilaya za sasa za mikoa miwili ya Manyara na Arusha za Kiteto, Simanjiro, Monduli, Ngorongoro na Londigo.

“Baadaye mwaka 1965 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Monduli. Mwaka 1967 aliteuliwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Uchukuzi na Kazi.

Mwaka 1970 alichaguliwa tena kuendelea kuwa Mbunge na pia akateuliwa na Rais kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais na baadaye mwaka 1972 akateuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mwaka 1975 aliendelea tena kushinda ubunge wa Monduli na akateuliwa tena kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Mwaka 1977 alichaguliwa kwenye Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya chama hicho kuungana na Afro-Shiraza Party (ASP) tarehe 5 Februari, 1977, chama kilichokuwa kikiiongoza Zanzibar wakati huo.

Tarehe 13 Februari, 1977, Rais Nyerere alimteua kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nafasi ambayo alidumu kuitumikia hadi tarehe 7 Novemba, 1980, alipojiuzulu na kwenda masomoni nchini Yugoslavia.

Hayati Sokoine alirejea nchini mwaka 1983 na kuteuliwa tena na Rais Nyerere kuwa Waziri Mkuu mnamo tarehe 23 Februari, 1983.

Hayati Sokoine aliitumikia nchi hadi tarehe 12 Aprili, 1984, alipofariki kwa ajali ya gari kwenye eneo la Dawaka, kilomita chache nje ya Morogoro, wakati akitoka bungeni Dodoma. Hayati Sokoine alikuwa na umri wa miaka 45 wakati alipofariki.