January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt. Samia aridhia mikopo ya asilimia kumi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dodoma

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameridhia kuanza kutolewa tena kwa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri zote nchini na itaanza kutolewa Julai, Mosi, 2024.

Mikopo hiyo ya asilimia 10 inatolewa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kote nchini.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Josephine Gezabuke, Bungeni jijini Dodoma.

Katimba amesema fedha kwa ajili ya mikopo hiyo ipo na Rais Samia tayari ameridha ianze kutolewa kuanzia Julai Mosi, 2024.

Katika swali lake, Gezabuke amesema wako vijana waliojiunga katika vikundi kwenye maeneo mbalimbali nchini lakini hawajapata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.

Mbunge huyo ametaka kujua kama Serikali ipo tayari katika kuwapatia mikopo hiyo iwape kipaumbele wanawake na vijana waliokuwa wameshajiunga katika vikundi.

Akijibu swali hilo, Katimba amesema; “Sasa hivi tunaendelea na maandalizi na niwahakikishie vijana wote, wanawake na watu wenye ulemavu wakae mkao wa kula, kuanzia Julai Mosi mwaka huu.”

Amesema kwa kipindi chote ambacho imesitishwa, halmashauri zilitenga fedha hizo, lakini marejesho kwa vikundi vilivyokuwa vikidaiwa yalikuwa yanaendelea na hivyo fedha za kutosha zipo.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu, Fakharia Shomari Khamis, alihoji Serikali ina kauli gani kuhusu utekelezaji wa wito wake kwa vijana kujiajiri au kujiunga katika vikundi ili kutambuliwa na kukopesheka kisheria.

Akijibu swali hilo, Katimba amesema mikopo hiyo imewezesha makundi ya vijana kupata mitaji kwa ajili ya kuanzisha na kuboresha shughuli zao za uzalishaji.

“Serikali inaendelea kutoa wito kwa vijana kutumia fursa zinazowalenga zikiwemo za elimu ya vikundi, mafunzo na ushauri wa kitaalamu kwa shughuli zinazofanywa na vikundi vya vijana, fursa ya mikopo inayotolewa katika mamlaka za Serikali za mitaa ili waweze kijikwamua kiuchumi,” amesema.

Uamuzi wa kusitishwa kwa mikopo hiyo ulitangazwa Aprili 13, 2023 bungeni na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ili kupisha utaratibu mwingine wa utoaji wa mikopo hiyo.

Hata hivyo Aprili 16, 2024, Waziri wa Tamisemi, Mohammed Mchengerwa, alitangaza kurejeshwa kwa mikopo hiyo wakati akisoma bajeti yake ya mwaka 2024/25.

Amesema halmashauri 10 za majaribio zitaanza utoaji wa mikopo hiyo kwa kutumia benki. “Mikopo inayotarajiwa kutolewa ni Sh227.96 bilioni ambapo sh. Bilioni 63.67 ni fedha za marejesho zilizokuwa zikiendelea kukusanywa kutokana na mikopo iliyotolewa kabla ya kusimamishwa.

Amesema sh. bilioni 63.24 ni fedha zilizokuwa zinatengwa kwa ajili ya mikopo na Sh101.05 bilioni ni fedha ambazo zimetengwa kutokana na makisio ya makusanyo ya mapato ya ndani ya mwaka 2024/25.