*Asema inatokana na NSSF kufanya mageuzi mbalimbali pamoja na kuwekeza vizuri kimkakati
Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Jeshi la Magereza kwa kufanya mageuzi na kukamilisha mradi wa kimkakati wa kiwanda cha sukari Mkulazi kilichopo Mbigiri Mkoani Morogoro.
Amesema kukamilika kwa mradi huo wa kimkakati kunatokana na NSSF kufanya mageuzi mbalimbali ikiwemo kuwekeza kimkakati, kujipanga vizuri na kuusimamia vizuri mradi huo. Mradi wa kiwanda cha sukari Mkulazi ulizinduliwa rasmi Agosti 7, mwaka huu, una uwezo wa kuzalisha tani 50,000 kwa mwaka na tayari uzalishaji wa sukari ya majumbani ulianza tarehe 1 Julai, 2024.
Mhe. Dkt. Samia alitoa pongezi hizo tarehe 28 Agosti 2024 wakati akifungua kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa taasisi za umma kilichofanyika Mkoani Arusha.
“Nilipokuwa kwenye ziara Mkoani Morogoro nilifungua kiwanda cha sukari Mkulazi cha NSSF wakishirikiana na Jeshi la Magereza; hawa waliwekeza kimkakati, lakini wamefanikiwa baada ya kufanya mageuzi mbalimbali…hongereni sana NSSF,” amesema Mhe. Rais Dkt. Samia.
Aidha, alishauri kuwekeza kwa kufanya upembuzi yakinifu kwenye miradi mbalimbali ili iweze kuleta tija zaidi.
Akifunga kikao kazi hicho, Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Moses Kusiluka amesisitiza umuhimu kwa viongozi kutekeleza kwa ukamilifu maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Rais Dkt. Samia wakati akifungua mkutano huo na kuwa Ofisi yake itahakikisha maelekezo hayo yanatekelezwa.
Dkt. Kusiluka pia amewataka wenyeviti na watendaji wakuu wa taasisi za umma kusimamia utendaji wa taasisi zao ili kuongeza ufanisi na tija hasa ukizingatia Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye taasisi hizo na inatarajia kupata manufaa kutokana na uwekezaji huo.
Aidha, ameiagiza Ofisi ya Msajili wa Hazina kutekeleza kikamilifu mfumo wa kupima ufanisi wa taasisi na mashirika ya umma kwa kuangalia matumizi sahihi ya rasilimali huku akisisitiza umuhimu taasisi zote kuhakikisha mifumo ya TEHAMA inasomana ili kurahisisha utendaji wa Serikali kufanyakazi pamoja.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja